Mkuu wa Mkoa wa Njombe Anthony Mtaka, amempokea Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, aliyefika mkoani hapa kwa ziara ya kujifunza kuhusu mbinu na mikakati iliyosaidia Njombe kupunguza viwango vya udumavu.

Ziara hiyo imehusisha viongozi mbalimbali kutoka Katavi, wakiwemo Wakuu wa Wilaya zote, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wenyeviti wa Halmashauri pamoja na wataalamu wa afya, kwa lengo la kujifunza mbinu bora za lishe na kupambana na udumavu.

Akizungumza wakati wa mapokezi, Mhe. Anthony Mtaka amemkaribisha Mhe. Mwanamvua Mrindoko na ujumbe wake kwa heshima kubwa, akisema

"Mkoa wa Njombe unayo furaha kubwa kuwapokea viongozi na wataalamu kutoka Katavi. Hii ni ishara kwamba jitihada zetu katika kupunguza udumavu zinatambulika kitaifa. Tunayo historia ya kushirikiana na mikoa mingine katika masuala ya maendeleo, na tuko tayari kushirikiana nanyi kuhakikisha tunapambana na udumavu kwa pamoja."

Rc Mtaka pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa kinara wa lishe nchini na kuweka msukumo mkubwa katika afua za lishe.

"Tunamshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake thabiti na dhamira yake ya kuimarisha lishe nchini. Uongozi wake umewezesha mkoa wetu kutekeleza afua mbalimbali za lishe, ambazo leo hii zimekuwa mfano kwa mikoa mingine. Ni kupitia jitihada hizi ndipo tumepata nafasi ya kushirikiana na Mkoa wa Katavi kwa lengo la kupambana na udumavu," alisema Mhe. Mtaka.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, ameushukuru Mkoa wa Njombe kwa mapokezi mazuri na kuwapongeza kwa jitihada zao katika mapambano dhidi ya udumavu.

"Tunawashukuru kwa kutupokea kwa moyo mkunjufu na kwa kushiriki nasi maarifa yenu. Njombe ni mfano wa kuigwa katika kupunguza udumavu, na tumejifunza mengi ambayo tutayatekeleza kwa vitendo Katavi. Tumeona ni kwa namna gani juhudi za pamoja kati ya serikali, jamii na wadau mbalimbali zimeleta matokeo chanya, na nasi tutafuata nyayo zenu," alisema Mhe. Mrindoko.












Share To:

Post A Comment: