Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) imezindua Kampeni ya kuhamasisha utalii wa ndani katika mapango ya amboni Tanga kuelekea sikukuu ya wapendanao inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 14 Februari.
Kampeni hiyo iliyozinduliwa na Mkuu wa Wilaya ya Tanga Mhe. Japhari Kubecha leo tarehe 26/01/2025, inaenda kwa kauli mbiu isemayo “Diko la Amboni: Furaha ya Asili,Utajiri wa Urithi,” ambapo pamoja na kuhamasisha utalii wa ndani kampeni hiyo inalenga kukuza uchumi wa wajasiriamali wadogo katika mkoa wa Tanga.
Akizunguza katika uzinduzi huo, Mhe. Kubecha aliipongeza uongozi wa NCAA kwa juhudi za kuhamasisha utalii wa ndani katika mapango hayo na kutoa rai kwa wananchi ndani na nje ya Mkoa wa Tanga kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vilivyopo ndani ya nchi.
“tunatambua juhudi za pekee zinazofanywa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kuhakikisha kuwa utalii mambo kale na urithi wa utamaduni unaendelea kuwa kivutio bora cha watalii nchini, kutokana na hili naomba nitoe rai kwa wananchi wote ndani na nje ya mkoa wa Tanga kuhakikisha kuwa siku ya tarehe 14, Februari tunakutana hapa Amboni”. Alisema Mhe. Kubecha.
Kwa upande wake Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, NCAA anayesimamia huduma za utalii na masoko, Mariam Kobelo alisema kwamba kuelekea siku hiyo NCAA itatoa nafasi kwa wakazi wa Tanga kushiriki kwenye shughuli mbalimbali zitakazo fanyika hapo ili kuendelea kutoa hamasa na kuongeza uwelewa wa shughuli mbalimbali za Uhifadhi zinazofanywa na Mamlaka hiyo.
“Shughuli hii ambayo tunaenda kuifanya msimu huu wa sikukuu za wapendanao itahusisha mashindano ya Upishi wa vyakula vya asili, ambayo yatafanyikia hapa amboni pamoja na kutembea ndani ya mapango na kupatiwa elimu juu ya kivutio hiki cha kipekee kilichopo katika nchi yetu” Alisema Mariam
Aidha, Kobelo alieleza kuwa ili kuhakikisha siku hiyo itakuwa nzuri na kuwezesha watanzania wengi kushiriki, Mamlaka imeshirikiana na Kampuni ya Utalii ya Smiles Safaris ambayo itatoa huduma za kuwaleta watalii amboni kutoka mikoa ya Dar es salaam, Arusha, Kilimanjaro na Tanga ambapo gharama za ushiriki kwa kila Mkoa zitatolewa na gharama hizo zitahusisha Chakula, Malazi siku moja, viingilio pamoja na picha.
Mapango ya Amboni Tanga yanayosimamiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) tangu mwaka 2019 na yapo umbali wa Km 9 tu kutoka katikati ya Jiji la Tanga.
Mapango hayo yamefanyiwa maboresho mbalimbali ikiwemo ufungaji wa taa maalum kuwezesha mgeni kuona vivutio vilivyopo ndani ya Mapango sambamba na kuboresha njia za mapito katika eneo la ndani ya mapango hayo ambapo kwa sasa eneo hilo linapokea wageni zaidi ya 30,000 kwa mwaka.
Post A Comment: