Sekta ya michezo ya kubahatisha nchini Tanzania imepiga hatua kubwa baada ya uzinduzi rasmi wa Bahati Nasibu ya Taifa Tanzania iliyopata baraka kutoka zote kutoka kwa Mhe. Hamad Chande, Naibu Waziri wa Fedha. Mpango huu, unaosimamiwa na ITHUBA, Kampuni inayoongoza barani Afrika katika kuendesha michezo ya Bahati Nasibu, unalenga kuleta mapinduzi katika sekta hiyo, kuchochea maendeleo ya kitaifa, na kutoa fursa kwa kila Mtanzania kushiriki.


"Leo ni siku ya kihistoria kwa Tanzania," alisema Mhe. Chande wakati wa hotuba yake. "Kwa kumkaribisha ITHUBA kama mwendeshaji rasmi wa Bahati Nasibu ya Taifa, tunatoa kipaumbele katika suala zima la uvumbuzi, uaminifu, na uwazi huku tukileta jukwaa litakalochochea ukuaji wa uchumi, ajira mpya, na miradi ya maendeleo ya kitaifa kwa ajili ya kuinua maisha ya wananchi."

Fursa za Kusisimua za Michezo kwa Wote; Bahati Nasibu ya Kitaifa itakuwa na mkusanyiko wa michezo mbalimbali ya kuvutia iliyoundwa mahsusi kwa ajili ya kuwashirikisha na kuwaburudisha Watanzania, ikiwa ni pamoja na LOTTO, TAMBA NA NAMBA, SPIN4CASH, na TOBOA CHAP CHAP. Tiketi zinaanzia bei ya Shilingi 100 tu za Kitanzania, kuhakikisha kila mtu anaweza kushiriki.

"Kila tiketi itakayouzwa itachangia kuboresha michezo, elimu, na miradi ya kijamii," aliongeza Mheshimiwa Chande. "Bahati Nasibu ya Taifa hii ni mfano wa jinsi michezo ya kubahatisha inavyoweza kutumika kama chombo cha maendeleo endelevu huku ikiwaletea washiriki furaha."

Ujumbe wa Afisa Mtendaji Mkuu wa ITHUBA Group, Bi. Charmaine Mabuza, ulisisitiza dhamira ya kampuni hiyo katika maendeleo ya Tanzania. "ITHUBA inajivunia kushirikiana na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT) kuendesha Bahati Nasibu ya Taifa. Dira yetu ni kutoa uzoefu wa hali ya juu wa michezo ya Bahati Nasibu kwa uwazi, kuburudisha, na kusaidia maendeleo endelevu. Bahati Nasibu hii si tu kuhusu michezo bali pia ni sehemu ya kuinua jamii zetu na kuwekeza katika mustakabali bora wa Tanzania."

Kwa usimamizi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Bahati Nasibu ya Taifa itazingatia viwango vya juu vya uwazi na haki. Balozi Modest J. Mero, Mwenyekiti wa GBT, alibainisha umuhimu wa uadilifu katika mpango huu. "Sifa ya ITHUBA katika uwajibikaji wa kimaadili na uvumbuzi unaifanya Kampuni hii kuwa mshirika bora. Bodi ya Michezo ya Kubahatisha itahakikisha Bahati Nasibu ya Taifa inafanya kazi kwa uwazi na uaminifu kama jukwaa salama linalochangia malengo ya kiuchumi ya Tanzania," alisema Balozi Mero.

Bahati Nasibu ya Taifa inatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya michezo ya kubahatisha nchini. Mapato ya tiketi yatatumika kufadhili maendeleo ya michezo katika ngazi ya msingi, uwezeshaji wa vijana, na miradi muhimu ya kijamii, kuimarisha jukumu la Bahati Nasibu ya Taifa kama chombo cha maendeleo ya kijamii.

Baadhi ya Michezo inayopatikana Kupitia Bahati Nasibu ya Taifa: LOTTO: Jakpoti za kila siku zenye zawadi kubwa zinazobadilisha maisha.
TAMBA NA NAMBA: Mchezo wa haraka wa droo kila baada ya dakika 5.
SPIN4CASH: Michezo ya kushinda papo hapo na malipo ya haraka.
TOBOA CHAP CHAP: Michezo ya papo hapo yenye mada za kuvutia kama MFUGA KUKU na TUNDA KITMATI.

Fursa kwa Wadau Wote: Washiriki: Zawadi za zaidi ya dola milioni 60 zinatarajiwa kutolewa katika mwaka wa kwanza pekee.
Wauzaji na Washirika wa Biashara: Kamisheni za takriban dola milioni 6.6, pamoja na mafunzo na msaada wa kimasoko.
Vyombo vya Habari: Zaidi ya dola milioni 3.5 zimetengwa kwa masoko na matangazo, ikijumuisha fursa za kipekee za maudhui.

Bahati Nasibu ya Taifa itahakikisha ushirikishwaji wa kila mmoja wetu kwa kutoa tiketi kupitia majukwaa ya kidigitali, huduma za simu, na vituo vya rejareja kote nchini. Juhudi za kufikia maeneo ya vijijini pia zimepangwa kuhakikisha kuwa hata jamii za pembezoni zinaweza kushiriki na kufaidika.

"Bahati Nasibu ya Taifa ni alama ya mshikamano, uwezeshaji, na maendeleo," alisema Bi. Mabuza. "Kwa pamoja, tunatengeneza urithi wa ustawi wa pamoja kwa vizazi vijavyo."







Share To:

Post A Comment: