Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Khamis Hamza Chilo, amempongeza Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo, kwa juhudi zake za kuwahudumia wananchi wa jimbo hilo.
Akizungumza Jumamosi, Januari 11, 2025, katika Hafla Maalumu ya Uhamasishaji na Kutoa Elimu ya Nishati Safi ya Kupikia kwa Viongozi wa Dini ya Kiislam, Chilo amesema kuwa wananchi wa Arusha walimchagua Gambo kwa imani na matumaini, na mbunge huyo ameonesha uwezo mkubwa wa kuwasemea bungeni.
“Gambo hatulii kwenye kiti chake bungeni. Muda wote yupo kwenye viti vya serikali kwa ajili ya kuwaombea huduma wananchi wake. Mara unamkuta kwa Waziri wa Afya, mara Waziri wa Fedha, nakadhalika. Anapigania changamoto za Arusha zitatuliwe, na wananchi wake waishi kwa raha zaidi,” amesema Chilo.
Aidha, Chilo amebainisha kuwa Gambo ana misimamo thabiti inayolenga kuwatetea wananchi wake na anapenda kushirikiana na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutambua mchango wake mkubwa katika kuboresha huduma jimboni Arusha.
“Yapo mambo mengi hayakuwepo kabla ya Gambo kuwa mbunge, lakini kupitia jitihada zake na kuyasemea serikalini na kwenye chama, leo huduma hizo zimepatikana. Wananchi wanaendelea kufurahia matunda ya uongozi wa Rais Samia,” ameongeza.
Hafla hiyo, iliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), iliandaliwa na Mbunge Gambo kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia. Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi wa serikali za mitaa jijini Arusha, Wajumbe wa Jumuiya ya Maridhiano, viongozi kutoka Wizara ya Nishati, watendaji kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), masheikh kutoka taasisi mbalimbali za dini ya Kiislamu, na wadau wa nishati safi nchini.
Post A Comment: