Naibu katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa(UN) Amina Mohamed ameipongeza serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mkakati wa kufanya utafiti wa kina wa kijiolojia na utafutaji madini nchini.
Naibu Katibu Mkuu Amina Mohamed ameyasema hayo leo wakati wa mkutano wa pembeni wa Mkutano wa Nishati alipokutana na Waziri wa Madini Anthony Mavunde
“Naipongeza Tanzania chini ya uongozi wa Mhe. Rais Samia ambao umekuja na ubunifu mkubwa katika maeneo mbalimbali.
Mpango wa kufanya utafiti wa kina kupitia Vision2030 ni mpango ambao tunauunga mkono kwa kuwa una lengo la kubaini madini ambayo mnayo na hivyo kujiapanga vyema juu ya uvunaji wa madini hayo.
Dunia hivi sasa ina mahitaji makubwa ya madini mkakati,Tanzania imebarikiwa kuwa na madini hayo kwa uwingi hivyo suala la uongezaji thamani,utunzaji wa mazingira na kulinda jamii zinazoishi katika maeneo ya uchimbaji wa madini ni vyema yakazingatiwa wakati wa uandaaji wa mkakati maalum wa uvunaji wa madini ya kimkakati.
Umoja wa Mataifa kupitia programu zake mbalimbali za utunzaji wa mazingira ipo tayari kuunga mkono jitihada hii kubwa ya serikali ya Tanzania“amesema Mhe. Mohamed.
Akizungumza katika mkutano huo,Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema kipaumbele cha sekta ya Madini kwa hivi sasa ni kufanya utafati wa kina ili kuiwezesha nchi kupata taarifa za kiwango na ubora wa madini iliyonayo.
Amongeza kwamba, utafiti wa kina utaleta matokeo chanya kwenye maeneo ya kijamii na kiuchumi na hivyo kusaidia kuchochea maendeleo ya Tanzania,kwakuwa pamoja na mafanikio yote ya kwenye sekta ya madini eneo ambalo limefanyiwa utafiti ni asilimia 16% ya eneo la nchi nzima.
Post A Comment: