Na Asia Singano, WF, Arusha.
Watoa huduma za fedha nchini wametakiwa kufuata Sheria na taratibu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ikiwemo kujisajili, kutoza viwango sahihi vya riba na kuwapa nakala za mikataba wakopaji baada ya wao kuelewa mkataba wa makubaliano ya kukopa na kusaini ili kuepuka adhabu mbalimbali zitakazotolewa kwa wanaokiuka Sheria za huduma za fedha.
Onyo hilo limetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Bw. Selemani Msumi, ofisini kwake alipokutana na kufanya mazungumzo na Timu ya Wataalamu wa kutoa elimu ya fedha kutoka Wizara ya Fedha na taasisi zake pamoja na wadau mbalimbali.
Alisema kuwa Serikali inaendelea kufanya uchunguzi kuwabaini wanaofanya biashara ya kutoa huduma za fedha bila leseni, huku akisisitiza kuwa watakaobainika kukiuka Sheria na taratibu za huduma ndogo za fedha hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
‘’Mtu yeyote anayeendesha biashara ya kukopesha pasipo kufuata taratibu, pasipokuwa na leseni hilo ni kosa na ni wizi kama wizi mwingine, tumeshaanza oparesheni ya kuhakikisha wanaokopesha bila kuwa na leseni na ambao hawafuati Sheria na taratibu tunawakamata’’ alisema Bw. Msumi.
Akitoa elimu ya fedha kwa wajasiliamali na wananchi wa Kata ya Ilikiding’a katika Shule ya Sekondari Ilikiding’a, Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw Salim Kimaro amewataka wajasiliamali hao kusajili vikundi vyao vya huduma ndogo za fedha ili kulinda fedha zao dhidi ya wanakikundi wasiyo waaminifu.
‘’Hatusemi vile vikundi vyenu ambavyo havijasajiliwa mvivunje hapana, ni vizuri ila nendeni mkavisajili, kama wale mliowaona kwenye filamu wangesajili kikundi chao na kuweka hela benki fedha zao zisingepotea’’ alisema Bw. Kimaro.
Kwa upande wake Bw. Lulu Mesikana, ambaye ni mmoja wa wajasiliamali waliohudhuria mafunzo hayo ya elimu ya fedha, aliipongeza Wizara ya Fedha kwa kuona umuhimu wa kutoa elimu hiyo kwa wananchi huku akiomba programu hiyo ya elimu ya fedha iwe endeevu.
‘’Tunashukuru sana kwa semina hii na tukitoka hapa sasa tutakuwa makini na tutalinda fedha zetu ili tusipate hasara kama walivyoibiwa fedha wale tuliowaona kwenye filamu ya elimu ya fedha’’ alisema Bw. Mesikana.
Naye Afisa Mwandamizi, Uchambuzi Fedha, Idara ya Sera, Utafiti na Mipango, kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA. Gladness Mollel, amewashauri wajasiliamali hao kuwekeza katika njia mbalimbali ikiwemo zile walizofundihswa na watalam wa elimu ya fedha kwa ajili ya kujikimu katika kila hali ya maisha.
‘’Kuna njia nyingi za uwekezaji ikiwemo hatifungani kuna aina mbalimbali za hatifungani, kwanza zipo hatifungani za Serikali na pia zipo hatifungani za kampuni na taasisi nyingine’’ alisema Bi. Gladness.
Post A Comment: