Serikali kupitia Wizara ya Afya imetenga kiasi cha Shilingi Milioni 600 ili kuipandisha hadhi Zahanati ya Suji iliyopo kijiji cha Malindi Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro kuwa kituo cha afya ambacho kitatoa huduma zaidi ikiwemo huduma za kulaza wagonjwa pamoja na chumba cha upasuaji wa dharura.
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Januari 8, 2025 akiwa katika ziara ya kukagua na kuzindua miradi ya sekta ya afya katika mkoa wa Kilimanjaro ambapo ameweka jiwe la msingi la zahanati hiyo.
"Tumeona ni vyema tukaipandisha hadhi zahanati hii ya Suji - Malindi kuwa kituo cha afya ili tuweze kuongeza huduma za afya ikiwemo wodi maalum za kulaza wagonjwa, chumba maalum cha upasuaji na eneo maalum la huduma za mionzi," amesema Waziri Mhagama.
Amesema, lengo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kutoa fedha zote hizo ambazo zinatokana na uongozi wake mahiri wa mashirikiano mazuri ya kidiplomasia ni kutaka wananchi wake kupata huduma za afya karibu na maeneo yao.
Amesema, zahanati hiyo ikikamilika na kupewa hadhi ya kuwa kituo cha afya itasaidia wananchi wa kijiji hicho kupunguza umbali za zaidi ya kilimeta 10 za kufuata huduma za afya ikiwemo huduma za kujifungua na upasuaji.
Aidha, Waziri Mhagama amewataka wananchi wa kijiji hicho kuitunza na kuiendeleza amani iliyopo, kutunza mazingira na miundombinu iliyopo, kuepuka uharibifu wa mazingira unaochochea mabadiliko ya tabia nchi na kusababisha kutokea kwa magonjwa ya milipuko pamoja na kuendelea kuchukua tahadhari juu ya magonjwa hayo kwa kuwasikiliza wataalam.
Aidha Waziri Mhagama ameendelea kuwakumbusha Watanzania juu ya kuacha tabia bwete kwa kufanya mazoezi, kuzingatia mlo bora kwa kupunguza matumizi ya mafuta, chumvi na sukari ili kuepuka magonjwa yasiyoambukiza.
Post A Comment: