Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amepongezwa kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi milioni 603.8 zilizofanikisha ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya Luhunga iliyopo Kijiji cha Mgombe Kata ya Nyakitonto Halmashauri ya Wilaya Kasulu.
Pongezi hizo zimetolewa hivi karibuni na Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu alipofanya ziara shuleni hapo na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo ambayo watoto wa kidato cha kwanza tayari wameshaanza masomo.
“Napenda kutoa shukrani kwa Mhe. Rais kwa kazi kubwa ya kuifungua Kigoma kwa kuiwezesha miundombinu mbalimbali lakini leo nitaongelea shule hii mpya ya Luhunga kupitia kiasi cha shilingi milioni 603.8 alichotoa ,” ameeleza Kanali Mwakisu.
Ameongeza : “ kilichonifurahisha madarasa tayari yameshakamilika na watoto tayari wapo darasani tokea Januari 13,2025 mwanzo walifikia shule mama ya Nyakitonto na leo wapo hapa ikiwa miundombinu ya kuwawezesha kukaa na kusoma ikiwa tayari,” amesema.
Pia, Kanali Mwakisu amewapongeza wasimamizi wa mradi huo kwa kushirikiana na wahandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kwa usimamizi mzuri walioufanya na kutoa wito wa utunzwaji wa miundombinu hiyo ili iweze kusaidia vizazi vingi.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Mgombe, Zabron Kigwe amesema kuwa uwepo wa shule hiyo utapunguza adha ya watoto kutembea umbali mrefu pamoja na vishawishi wanavyokumbana navyo njiani hasa kwa watoto wa kike pamoja na kutoa ahadi ya kuhakikisha shule inakuwa bora ili wanafunzi waweze kutimiza ndoto zao.
Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo walioongea na mwandishi wetu wamemshuru Mhe. Rais kwa kufanikisha ujenzi wa shule hiyo kitu wanachoamini kitasaidia kwakiasi kikubwa maendeleo ya Kijiji cha Mgombe siku za mbeleni.
Post A Comment: