Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kiseo Yusuf Nzowa,akipeperusha béndera kama ishara ya kuzindua mbio za Kilimanjaro Premium Lager International Marathon 2025 katika hoteli ya Salinero-Kilimanjaro huku wadhamini wa mbio hizo na wadau wengine wakishuhudia uzinduzi huo.
Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) Khensani Mkhombo akizungumza wakati wa uzinduzi huo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kiseo Yusuf Nzowa akizungumza wakati wa tukio hilo.
MSIMU wa 23 wa mbio za kimataifa za Kilimanjaro Premium Lager International Marathon 2025 umezinduliwa mkoani Kilimanjaro hafla iliyowakutanisha wadau mbalimbali wa michezo.
Mbio hizo zimezinduliwa mwishoni mwa wiki hii katika Hoteli ya Salinero mkoani humo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro Kiseo Yusuf Nzowa, akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu,ametoa pongezi nyingi kwa wadhamini, wandaaji na wadau wengine wa michezo kwa kufanya mashindano hayo kuwa endelevu, jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa kuweka Mkoa wa Kilimanjaro katika ramani ya dunia.
Yusuf anasema mbali na kukuza afya za watu, mbio hizo ambazo sasa ni maarufu Barani Afrika zinachangia kukuza uchumi wa mkoa na Taifa kwa ujumla kupitia sekta ya utalii kila mwaka, kutokana na washiriki wa ngazi zote kuwepo mkoani humo kipindi chote cha mbio hizo.
“Tunajivunia mbio za Kilimanjaro Premium Lager International Marathon ambazo zimeendelea kuwa maarufu kila mwaka; tukio hili kwa sasa limekuwa maarufu huku likishirikisha zaidi ya watu 12,000 na idadi kama hiyo ya mashabiki wanaokuja mkoani kwetu kwa ajili ya kufuatilia”, amesema
Ameongeza, "tukio hili linawaleta pamoja watu kutoka takribani nchi 56 jambo ambalo linayafanya mashindano hayo kuwa ya kipekee ukanda wa Afrika Mashariki na Kati,"
Yusuf alitoa rai kwa wadau wote wa michezo kushirikiana kwa karibu na waandaaji wa mbio hizo ili ziendelee kuleta manufaa zaidi ya kiuchumi kwa Mkoa, Taifa na kwa mtu mmoja mmoja kutokana na ukweli kwamba mashindano hayo yanazidi kukua na sambamba na umaarufu wake kuendelea kukua kila mwaka.
"Mbio hizi huandaliwa kila mwaka na mwaka huu ni msimu wake wa 23, manafuaa yake kiuchumi yanaonekana wazi kwa jamii yote ya Watanzania, kutokana pamoja na mambo mengine ikiwemo kukua kwa biashara mbalimbali katika mji wa Moshi; nitoe wito kwa wafanyabiashara wote wa Moshi na Mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla kuhakikisha wanazingatia ubora katika kutoa huduma zao ili kulinda heshima ya Mkoa katika nyanja za kibiashara”, amesema.
“Nichukue fursa hii kuwapongeza wadhamini wote wa mbio hizi wakiongozwa na mdhamini mkuu Kilimanjaro Premium Lager ambao wanadhamini mbio za kilomita, kampuni ya YAS ambao wanadhamini mbio za kilomita 21 (Yas Half Marathon) pamoja na Benki ya CRDB ambao wanadhamini mbio za kilomita 5”, amesema
Anaongeza, “Napenda pia kuwaponegza wadhamini wengine ambao wanaunga mkono mbio hizo ambao ni pamoja na kampuni ya saruji ya Simba (Simba Cement), Kilimanjaro Water, TotalEnergies, kampuni ya TPC Sugar Ltd, Wasambazaji rasmi GardaWorld, CMC Automobiles, Salinero- Kilimanjaro, Kibo Palace Hotel na Keys Hotel, ambao ushiriki wao umechangia kuendelea kukua kwa mbio hizi”.
Akiongea katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Khensani Mkhombo, amesema kuwa kampuni hiyo inajivunia kuwa wadhamini wa mbio hizo kwa miaka 23 iliyopita kupitia Bia ya Kilimanjaro Premium Lager na kuifanya kampuni hiyo kuwa mmoja wa wadhamini wa muda mrefu kwenye tukio moja la kimichezo hapa nchini.
“Kutokana na mbio hizi kuzidi kupata umaarufu, Mwaka huu, kamati ya maandalizi ya mbio hizi imekuja na mkakati mpya unaolenga kufanya matamasha ya utangulizi ambayo yatafanyika siku za mwisho wa wiki kuelekea mbio hizi, ambapo matamasha hayo yataanza Ijumaa na kumalizika Jumapili ambayo ndiyo siku ya mbio hizo”, amesema
Akizungumzia zawadi zilizoandaliwa kwa msimu wa 2025, Mkhombo amesema kuwa Kilimanjaro Premium Lager imetenga jumla ya shilingi milioni 30, ambapo washidi wa kilomita 42 kwa wanaume na wanawake kila mmoja anatarajiwa kupata zawadi shilingi milioni 5.5, ambapo wanariadha wa Kitanzania ambao watashika nafasi ya kwanza katika mbio za kilomita 42watapata bakshishi ya 550,000/- kila mmoja.
Akizungumzia mafaniko mengine, Mkhombo amesema mbali na kukuza sekta ya michezo, mashindano hayo pia yameimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya wadhamini, wandaaji, chama cha riadha nchini RT pamoja na jamii yote kwa ujumla.
Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Biashara YAS, Isack Nchunda amesema, "Mwaka huu tunaadhimisha na kujivunia kuwa sehemu ya udhamini wa mbio hizi maarufu Barani Afrika kwa muongo wa kumi sasa, kupitia udhamini wetu wa mbio za kilomita 21 maarufu kama Yas Half Marathon, ambapo kitengo hiki kinawaleta washiriki takribani 6,500, wakiwemo wanariadha maarufu Barani Afrika”.
Amesema mwaka huu, wakimbiaji na washiriki wengine wa pembeni kwa maana ya mashabiki wa mbio hizo watarajie kuona mambo mazuri kwenye mbio za kilomita 21 kutokana na uzoefu walionao wadhamini wambio hizo ambao ni Yas, ambapo alitoa rai kwa washiriki wa mbio hizo kujitokeza mapema ili kuwahi nafasi zao kabla mbio hizo hazijaanza siku ya tukio hilo.
Kwa upande wake, Meneja Biashara wa Benki ya CRDB Kanda ya Kaskazini, David Peter, amesema kampuni hiyo inajivunia kuwa mmoja wa washiriki wa Karibu wa mbio hizo maarufu kupitia udhamini wake katika mbio za kilomita 5 za mashindano ya Kilimanjaro Marathon ambayo yanalenga kuboresha afya za watu sambamba na kukuza uchumi wa Mkoa wa Kilimanjaro na Taifa kwa ujumla.
“Kwetu hili ni jukwaa sahihi la kuitangaza benki yetu kwani tunatarajia kuwafikia Watanzania wengi wa Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro pamoja na wale Mikoa ya jirani kupitia udhamini wetu wa mbio za Kilomita 5 za Benki ya CRDB,” amesema na kuongeza, nitoe wito kwa washiriki kujisajili kwa wingi ili waweze kushiriki kitengo cha mbio za CRDB Bank kilomita 5.”
Kwa upande wao kamati ya waandaaji wa mbio hizo wamewashukuru wadhamini wakuu wa Kilimanjaro Premium Lager na YAS kwa kutenga kitita cha jumla ya shilingi milioni 53 ambazo zitatolewa kama zawadi ya Mbio za kilomita 42 na kilomita 21, pamoja na vitengo vinmgine mbalimbali.
Waandaaji hao pia wamesema kuwa tukio hilo mwaka huu, pia linalenga kuchangia asilimia 5 ya kila malipo ya kiingilio kwa ajili ya msaada kwa Shirika la Tumaini la Maisha (TLM), msaada ambao wamesema unalenga kuwahudumia watoto wanaougua ugonjwa wa saratani ili wapate matumaini mapya baada ya kupata matibabu ya ugonjwa huo.
“Pesa zote ambazo zitachangwa kwa ajili ya msaada huo mwaka huu, zitaelekezwa kwenye Kituo cha Matibabu ya saratani wka watoto kilihcoko katika hospitali ya rufaa ya kanda ya KCMC (KCMC ZRH) iliyoko Moshi, mkoani Kilimanjaro”, imesema sehemu ya taarifa ya wandaaji hao.
Mbio za Kimataifa za Kilimanjaro Premium Lager Marathon zinatarajiwa kufanyika Jumapili ya Februari 23, 2025, katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), ambapo mbio hizo zimeadnaliwa na kampuni ya Kilimanjaro Marathon na kuratibiwa hapa nchini na kampuni ya Executive Solutions Limited, ambapo kampuni ya Wild Frontiers ndiyo inawajibika na matayarisho yote ya usafiri pamoja na maswala yote ya masoko yanayohusiana na tukio hilo muhimu.
Post A Comment: