Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo, amesisitiza umuhimu wa umakini, mshikamano, na kipaumbele kwa miradi yenye tija kwa Taifa katika maandalizi ya bajeti ya mwaka wa fedha 2025\/2026.
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi TFS Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi TFS anayesimamia Kurugenzi ya Huduma Saidizi, Emanuel Wilfred, amesema mafanikio ya bajeti ya TFS yanategemea mipango shirikishi inayozingatia rasilimali zilizopo.
Akihutubia katika kikao cha maandalizi na mapitio ya bajeti ya TFS kwa mwaka wa fedha 2025\/2026, Kamishna Msaidizi Wilfred alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha bajeti hiyo inalingana na malengo ya taasisi na inafaidi Taifa kwa ujumla.
Aidha, aliwasihi washiriki kuhakikisha bajeti wanayoandaa inatekelezeka na inakidhi mahitaji ya taasisi na wananchi.
"Mshikamano na uwajibikaji wa pamoja ni msingi wa mafanikio. Tujitahidi kufanikisha malengo ya bajeti ya mwaka 2024\/2025 na kuandaa bajeti bora kwa mwaka 2025\/2026," alisisitiza.
Sambamba na hilo, alibainisha masuala sita muhimu ambayo washiriki wa kikao hicho wanapaswa kuyazingatia katika maandalizi ya bajeti kuwa ni Kumaliza Miradi Inayoendelea, Udhibiti wa Vihatarishi, Ufuatiliaji wa Maagizo na Masuala Muhimu, Kuimarisha Uwezo wa Mapato, Kusimamia Uvunaji Haramu wa Rasilimali za Misitu, Utekelezaji wa Mpango Mkakati wa TFS.
Aidha, washiriki walikumbushwa kuwa bajeti ya mwaka huu ni hatua ya mwisho ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa TFS wa 2021\/2022 – 2025\/2026. Hivyo, ni muhimu kuhakikisha majukumu yote yaliyopangwa yanakamilika kwa wakati.
Prof. Silayo aliwataka watumishi wa TFS kuimarisha mshikamano katika maeneo yao ya kazi na kushirikiana na taasisi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama, ili kuboresha utekelezaji wa majukumu ya Serikali kwa ujumla.
Post A Comment: