Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango imempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kwa juhudi anazozifanya za usimamizi mzuri wa miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa ndani ya Halmashauri hiyo.
Pongezi hizo zimetolewa na wajumbe wa kamati hiyo ambao ni waheshimiwa Madiwani, waliofanya ziara ya kukagua shughuli mbalimbali za ujenzi zinazoendelea katika shule ya Sekondari Mwakata, ambapo ujenzi wa jengo la utawala unaoendelea utagharimu kiasi cha Tsh. 103,520,000. Kwa sasa ujenzi wa jengo hilo upo katika hatua za umaliziaji wa jengo.
Aidha, kamati hiyo ilifanya ukaguzi katika shule ya Sekondari Isaka na kuona shughuli zinazoendelea za ujenzi wa bwalo la chakula, mabweni mawili na matundu 10 ya vyoo. Miradi hii katika shule ya sekondari Isakaa inagharimu kiasi cha Tsh. 374,000,000
Wakati wa ziara hii, Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo Mh. Ibrahim Six amewataka wakandarasi kuhakikisha wanamaliza ujenzi kwa wakati kama ilivyo kwenye mikataba yao ili majengo hayo yaweze kutoa huduma kwa wakati.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala Leonard Mabula amewasisitiza wakandarasi hao kuzingatia muda wa ukamilishaji wa majengo hayo ili yaweze kuhudumia wanafunzi kwa wakati.
Post A Comment: