Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mheshimiwa Edward Mpogolo, amesema Wilaya ya Ilala imejipanga kikamilifu kupokea ugeni mkubwa wa marais na viongozi wa nchi za Afrika wanaotarajiwa kuwasili nchini kwa ajili ya mkutano  utakaofanyika tarehe 27 na 28 Januari mwaka huu.

Ameyasema hayo leo, tarehe 25 Januari 2025, wakati wa zoezi la usafi wa mazingira lililoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, eneo la Terminal One.

Mheshimiwa Mpogolo amesema kuwa maandalizi yamefanyika kwa ushirikiano mkubwa kati ya serikali na mashirika binafsi kuhakikisha kila jambo linafanikiwa.

  Ameeleza  kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeweka mkazo mkubwa kwenye usafi wa mazingira ili kuhakikisha jiji linaakisi taswira nzuri ya nchi kwa wageni hao wa heshima.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza  umuhimu wa kushirikiana kwa vitendo katika kufanikisha tukio hilo kubwa. 

“Hii ni fursa adhimu kwetu wananchi wa Ilala  na Tanzania kwa ujumla. Tunapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa kuwa na  ukarimu, usafi, na mshikamano. Hivyo niwaombe kutoa ushirikiano na jeshi la police kuhakikisha usalama na amani vinakuwepo muda wote “ alisema Mheshimiwa Mpogolo.

Mwisho Mhe. Mpogolo amesema kuwa  kwa kusema kuwa hii ni nafasi muhimu ya kuipa Wilaya ya Ilala na Tanzania kwa ujumla nafasi ya kujitangaza kimataifa kama eneo la amani, maendeleo, na mshikamano wa kidiplomasia.









Share To:

Post A Comment: