MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewataka wakuu wa shule za sekondari wilayani humo, kufanya kazi kwa ushirikiano, weredi, busara, hekima na kusimamia maadili ya wanafunzi shuleni ili kuinua taaluma na ufaulu mzuri.
Aidha amesema katika kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka huu, jukumu kubwa la walimu ni kuhakikisha ufaulu unaongezeka kwani wazazi wanahitaji matokeo mazuri.
Amesema serikali chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, imeboresha kwa kiasi kikubwa mazingira ya kutolea elimu, hususan ujenzi wa shule, ukarabati na vifaa vya kufundishia.
Amesema Rais Dk. Samia katikaWilaya ya Ilala alielekeza sh. bilioni 35 kwa upande wa sekondari, ambapo kazi kubwa imefanyika ukiwemo ujenzi wa shule za kisasa za ghorofa.
Ameyasema hayo, jijini Dar es Salaam, alipokuwa akifunga mafunzo kwa walimu wakuu wa shule za sekondari za serikali, binafsi , maofisa watendaji wa kata 36 za Wilaya ya Ilala na wadau wa elimu.
Mpogolo amewataka wakuu hao wa shule kuwashirikisha kikamilifu walimu wa kawaida katika masuala mbalimbali yanayosaidia kuinua taaluma badala ya kuwatenga na kuwanyima nafasi hususan katika vikao muhimu.
“Wapeni nafasi kwa sababu mafanikio ya shule yanachangiwa na walimu hao lakini sifa mnapata ninyi wakuu wa shule, Ofisa Elimu, Mkurugenzi wa Halmashauri na mimi Mkuu wa Wilaya,”ameeleza Mpogolo.
Amesisitiza uhusuano mzuri miongoni mwa wakuu wa shule, walimu wakuu wa idara na watumishi wa halmashauri na kuheshimiana hata bila ya kufahamiana kiundani.
“Kuna wakati mwalimu anakuwa na changamoto, anatuma ujumbe wa kuomba ruhusa, mkuu wa shule unausoma halafu hujibu. Au mwalimu anamtumia ujumbe Ofisa Utumishi naye anausoma lakini hajibu. Hii haifai,”amesema Mpogolo.
Pamoja na hilo, Mpogolo aliwataka walimu kusaidia kusimamia maadili ya wanafunzi kwani wapo wanafunzi watukutuku wanao tembea na visu, mikasi, mawe, viwembe na bisbisi katika mabegi yao hivyo kutishia usalama.
“Ikiwezekana tutumie hata polisi kata kuwapekua wanafunzi hawa. Nyie walimu ndiyo mnakaa na watoto kwa kipindi kirefu kuliko mzazi na kuna wazazi wanaogopa kuwaeleza ukweli watoto wao. Tusaidie kulinda maadili ya watoto hawa,”amesema Mpogolo.
Aidha Mpogolo amewataka wakuu wa shule kuwapa maelekezo sahihi wazazi pindi wanapotaka kuwahamishia watoto katika baadhi ya shule maalumu.
“Mzazi anang’ang’ania kumhamishia mtoto katika shule maalumu wakati hana vigezo.Ana kuja kwako mkuu wa shule na wewe unamhakikishia nafasi ipo ila unamwelekeza aende kwa viongozi wa juu wampe ‘kimemo’ tu akuletee huku ukijua wazi jambo hilo haliwezekani,”amesema Mpogolo.
Aliwapongeza walimu kwa utendaji wao na kwamba serikali itaendelea kuwapa ushirikiano mkubwa katika kuwajengea mazingira bora ya kiutendaji kwa lengo la kuongeza ufaulu.
Awali Ofisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Mussa Ally, alisema jumla ya washiriki katika mafunzo hayo ni 121 na yalilenga kukumbushana majukumu katika kuinua taaluma.
Post A Comment: