Na Fredy Mgunda, Iringa.
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Iringa Vijijini, kimesema kinamuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, kutokana na mafanikio makubwa aliyoyapata katika sekta mbalimbali ndani ya kipindi kifupi tangu alipoingia madarakani.
Akizungumza na makatibu wa wenezi wa wilaya hiyo, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Wilaya ya Iringa Vijijini, Anord Mvamba, alisema kuwa Rais Samia amefanya mageuzi makubwa kwenye sekta ya afya, elimu, miundombinu ya barabara, upatikanaji wa maji, na kilimo, hivyo wananchi wa wilaya hiyo wameona ni muhimu kumuunga mkono katika kipindi cha pili cha uongozi wake.
“Katika kipindi cha uongozi wake, Rais Samia ameboresha huduma za afya na elimu, ameongeza miundombinu ya barabara na amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama. Hivyo, ni lazima tuwe na imani naye na tushirikiane kwa pamoja kumuunga mkono kugombea urais mwaka huu,” alisema Mvamba.
Aidha, viongozi, wananchi na wanachama wa CCM wilaya hiyo wameungana kutoa msaada wa kipekee kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho, ili waweze kuchagua viongozi watatu muhimu kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Mvamba pia aliwataka viongozi wa chama hicho kuendelea kutoa taarifa sahihi kuhusu mafanikio ya serikali, huku akisisitiza umuhimu wa kusema mema na mazuri yanayofanywa na Rais Samia na serikali yake.
Post A Comment: