Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa ametoa wito kwa Wahariri na Waandishi wa Habari kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Vyombo vya Usalama katika utekelezaji wa mikakati ya mawasiliano na programu kumi zilizopangwa kutekelezwa katika kipindi cha miaka miwili.
Ameeleza Kampeni hizo ni pamoja na usalimishaji silaha kwa hiari kwa kipindi cha msamaha wa Rais kinachotolewa kwa mujibu wa sheria pamoja na kampeni za uhamasishaji wa jamii kuwakubali wafungwa walioachiwa kwa msamaha.
Bashungwa ametoa wito huo, leo tarehe 13 Januari 2025 katika kikao kazi chake na Wahariri wa Vyombo vya habari kilicholenga kujadili utekelezaji wa Mikakati sita ya Mawasiliano ya Wizara na Vyombo vya Usalama katika kipindi cha miaka mwili.
Ameeleza kuwa Wizara kupitia Vyombo vya Usalama itaendesha kampeni ya usalama barabarani, kuelimisha wananchi suala zima la kufuata sheria na taaratibu za usalama barabarani sambamba na kampeni kuhusu tahadhari ya kinga na moto.
“Kampeni zote hizi, zitatekelezwa kwa muda wa miaka miwili, niwaombe Wahariri na Waandishi wa Habari, kutumia kalamu zenu katika kuelimisha umma kufuata kampeni hizi hususan, sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali na vifo vinavyoweza kuepukika” amesisitiza Bashungwa
Aidha, Bashungwa amebainisha kampeni ya kutokubaliana na wahamaiji haramu kupitia ushirikishwaji wa wananchi inayoitwa Mjue Jirani yako na urejeaji wa wakimbizi kwa hiari kwenye nchi zao.
Ameeleza kampeni nyingine ni utolewaji wa Vitambulisho vya Taifa, kuhamasisha jumuiya za kijamii kufuata sheria za usajili na Kuelimisha jamii kuhusu kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu.
Kadhalika, Bashungwa amesema kuwa Wizara na Vyombo vya Usalama itaboresha utoaji wa taarifa kwa umma, mara tu matukio yanapotokea ili kuondoa taharuki zisizo za lazima ili kuepusha wananchi kutoa taarifa zisizo sahihi.
Kwa Upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo amewashukuru Wahariri na Waandishi wa habari kwa kuendelea kuipa ushirikianao Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani, Vyombo vyote vya Usalama pamoja na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Nae, Mwenyekiti Jukwaa la Wahariri Tanzania, Deodatus Balile ameeleza Mwandishi wa habari ana nafasi kubwa katika jamii kwa kutoa elimu na taarifa inayowezesha jamii kuwa na ufahamu pamoja na kuiepusha na mambo mbalimbali.
Post A Comment: