Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa ameitaka Idara ya Uhamiaji kuendelea kuwa mstari wa mbele kuchochea na kukuza utalii nchini kwa kutoa huduma bora na nzuri kwa wageni wanaokuja nchini kwa shughuli mbalimbali.

Ameeleza hayo Januari 10, 2025 Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba, Zanzibar wakati alipotembelea ujenzi wa Bandari ya Shumba Mjini ambapo awali ilikuwa bandari bubu iliyotumiwa wananchi wageni kwenda bandari ya Mombasa, Kenya 

“Tuendelee kujipanga na kuhakikisha tunakuwa na huduma nzuri ya kuwapokea wageni ili  wakija wakafanya utalii watachangia utalii lakini wakipata huduma nzuri, wao pia wanaenda kuwa wasemaji wetu wazuri huko wanakotoka”

Bashungwa amesisitiza kuwa Idara ya Uhamiaji ikitoa huduma nzuri kwa wageni na watalii wanaaoingia nchini, hali hiyo itaendelea kuitangaza nchini yetu kwa Mataifa wanapotoka.

Aidha, Bashungwa ametoa pongezi kwa Mhe. Dkt Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kazi kubwa ya maendeleo anayoendelea kuifanya kwa kuifungua Zanzibar kiuchumi.

Kadhalika, Bashungwa ameeleza kukamilika kwa ujenzi wa Bandari ya Shumba Mjini itasaidia kukuza uchumi na kuwawezesha Wananchi na wageni kuingia na kutoka Zanzibar.

Awali, Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar, Hassan Ali Hassan ameeleza kabla ya kuanza ujenzi wa Bandari hiyo wananchi wa Kisiwa cha Pemba walitumia eneo hilo kwenda Mombasa Kenya bila utaratibu ambapo kukamilika kwa bandari hiyo itawezesha kusafiri kufuata sheria na taratibu.

Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Post A Comment: