Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega amemtaka Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Arusha Eng. Reginald Massawe kumsimamia kikamilifu mkandarasi Stecol Corporation anaejenga barabara ya Mianzini-Ngaramtoni Km 18 kuhakikisha inakamilika ifikapo Septemba mwaka huu.
Akizungumza wakati akikagua maendeleo ya ujenzi huo amesisitiza kufanyakazi usiku na mchana mpaka mradi huo ukamilike kwa wakati ili kurahisisha usafiri na usafirishaji jijini Arusha.
Amesisitiza ujenzi wa Barabara katika miji na majiji uendane na uwekaji taa za barabarani zinazotumia jua (solar power), ili kupendezesha mitaa na kuiwezesha kupitika wakati wote.
"Mh.Rais Samia ametoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya barabara jijini Arusha hivyo hakikisheni kazi inafanywa kwa ubora, hatutakubali barabara iharibike baada ya muda mfupi ", "amesisitiza Ulega.
Aidha, Waziri huyo amemhakikishia mkuu wa mkoa wa Arusha Paul Makonda kuwa Serikali itazijenga barabara zote unganishi na wezeshi jijini Arusha ili kupunguza msongamano wa magari na kuendana na maandalizi ya mashindano ya kombe la mataifa ya Africa AFCON 2027.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara jijini Arusha nakusisitiza itachochea ukuaji wa sekta ya utalii na kukuza uchumi wa watu jijini humo.
#KAZIINAONGEA
Post A Comment: