Balozi wa Marekani nchini, ambaye amemaliza muda wake, Michael Battle, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa dhamira yake katika kuleta maendeleo Tanzania lakini pia kwa utayari wake katika shughuli za ushirikiano.

Ikumbukwe kuwa, Rais Samia katika kipindi cha miaka mitatu ya utawala wake, amekuwa mstari wa mbele katika kutengeneza ushirikiano mzuri na Mataifa mbalimbali, ambapo pia jitihada hizo za kuwepo ushirikiano, zimesaidia kufungua fursa katika Sekta ya Uwekezaji na Utalii nchini.

Akiongea wakati akiagana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki baada ya kumaliza muda wake, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, 09, Januari, 2025,  Balozi Michael Battle amesema kuwa, Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, unafurahishwa na jitihada za Rais Samia na kwamba, ni vyema ushirikiano baina ya nchi hizi mbili ukaendelea kudumu.

Aidha, ameiomba pia Wizara ya Mambo ya Nje, kumpa ushirikiano wa karibu Kaimu Balozi atayekuwepo wakati Marekani ikingoja kutuma Balozi mwingine.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amesema kuwa, 

Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano kwa Ubalozi wa Marekani nchini na kuahidi kumpatia ushirikiano wa karibu Balozi ajaye katika utekelezaji wa majukumu yake awapo Tanzania, pamoja na kuangazia maeneo ya kuongeza wigo wa ushirikiano kwa manufaa ya nchi zote mbili.

Waziri Kombo amemshukuru Balozi Battle kwa ushirikiano mzuri kati ya Wizara na Ubalozi katika kipindi chote cha uongozi wake pamoja na kufanya kazi kwa karibu na Sekta na Wizara mbalimbali za kimaendeleo nchini.

Aidha, ametumia fursa hii kutoa salamu za pole kwa msiba wa Rais Mstaafu wa Marekani, Hayati Jimmy Carter aliyefariki Dunia Desemba 29, 2024.

KAZIINAONGEA

Share To:

Post A Comment: