Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, na Uratibu Mheshimiwa Ummy Nderiananga ametoa wito kwa vijana nchini kuchukua hatua madhubuti katika kujua hali zao za maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU).

Ametoa wito huo tarehe 30 Novemba, 2024, wakati akihitimisha wiki ya vijana katika uwanja wa Majimaji Mkoani Ruvuma katika kuelekea Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yanayofanyika kitaifa Mkoani Ruvuma.



Katika hotuba yake, Naibu Waziri Mhe. Nderiananga amebainisha kwamba, changamoto kubwa inayowakumba vijana ni ukosefu wa mwamko wa kupima afya zao, na kutokujua hali zao za maambukizi.

Amesisitiza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imejipanga kikamilifu kuendelea kuwaunga mkono vijana katika mapambano dhidi ya maambukizi ya VVU.


Akiwahimiza vijana kuendeleza mshikamano na juhudi za pamoja, Naibu Waziri amesema, ifikapo mwaka 2025, Wamelenga kuvuka malengo katika kupambana na janga la UKIMWI.

Aidha amesema ni muhimu kwa kila kijana kushiriki kikamilifu katika kupima afya, kujikinga na kuelimishana kuhusu athari za VVU.


Pamoja na hayo Mhe. Nderiananga amewataka vijana kushirikiana na Serikali, Mashirika ya Kiraia, na wadau mbalimbali kuhakikisha elimu kuhusu VVU na UKIMWI inafikia maeneo yote, hasa vijijini, ambako changamoto ya uelewa bado ni kubwa.


Haya yote yanafanyika ikiwa ni kuelekea Kilele cha Maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani ambapo huazimishwa kila Disemba Mosi ya mwaka, ambapo mwaka huu Kitaifa yanaadhimishwa Mkoani Ruvuma, yenye kauli mbiu isemayo: "Chagua njia sahihi, tokomeza UKIMWI"
Share To:

Post A Comment: