Waziri Mkuu, Mhe.Kassim Majaliwa amekemea utaratibu wa uwekaji wa Vizuizi na vituo vya ukaguzi barabarani bila kuzingazia tahadhari ya usalama kwa watumiaji wengine wa barabara.

Waziri Mkuu amekemea utaratibu unaofanywa na baadhi ya Halmashauri kuweka vizuizi na vituo vya ukaguzi kwa kuziba barabara bila ya kuzingatia matumizi sahihi ya barabara na hivyo kusababisha ajali.

Ameeleza hayo, leo Disemba 06, 2024 jijini Arusha wakati akifungua Kongamano la Kimataifa la 14 la Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET), na kusisitiza kuwa mwenye dhamana kutoa kibali cha kuweka vizuizi na vituo vya ukaguzi ni Jeshi la Polisi.

“Jeshi la Polisi kaeni na Halmashauri, vizuizi vyao barabarani vinasababisha ajali, hakuna sababu ya Halmashauri kuweka kizuizi cha kuzuia magari, mwenye kibali hicho ni Jeshi la Polisi peke yake kwa ajili ya ukaguzi wa usalama”, amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.

Waziri Mkuu ameeleza kuwa kuna baadhi ya Halmashauri zimeweka vizuizi barabarani kwa ajili maafisa kukusanya mapato ambapo utaratibu huo umekuwa ukiathiri watumiaji wengine wa barabara na kusababisha ajali katika maeneo hayo.

Aidha, Waziri Mkuu  amewataka Wahandisi na wataalamu wa miundombinu kuwa kiungo muhimu katika utekelezaji wa maelekezo hayo kwa kuendelea kutoa mapendekezo ya kitaalamu ya matumizi sahihi ya barabara ili kuhakikisha kuwa dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuifanya Tanzania kuwa salama zaidi kwa wote inatimia na inapewa kipaumbele.







Share To:

Post A Comment: