Na Ashrack Miraji
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe, Balozi.Dkt. Pindi Chana ( Mb) amezitaka Halmashauri za wilaya zote nchini kuanzisha matamasha ya Utalii na Uhifadhi huku akielekeza suala la kuwalinda wananchi dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu kuwa ajenda ya kudumu.
Mhe. Chana ametoa kauli hiyo leo Desemba 21, 2024 wakati akimwakilisha Mhe. Waziri Mkuu kufungua rasmi msimu wa pili wa Tamasha la Utalii la Same ambapo pia ametoa zawadi na tuzo kwa wadau mbalimbali kutambua mchango wao katika kufanikisha Tamasha hilo
"Wakati leo tunasherekea Tamasha la pili la Utalii la Same ni lazima tuhakikishe tunawalinda wananchi kutokana na wanyama wakali wakati huo huo tunahifadhi rasilimali tulizopewa na Mwenyezi Mungu ili zitusaidie kutuletea watalii zaidi " amefafanua Mhe Chana.
Amesema Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI na wananchi itaendelea kuhifadhi rasilimali kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Aidha amefafanua kuwa usemi wa kiswahii usemao "Tunza mazingira yakutunze" unadhihirisha kuwa mazingira yakitunzwa vizuri ikiwemo misitu na maliasili yatasaidia kujenga uchumi.
"Tukitunza mazingira tutapata mvua, tutapata maji, tutalima, tutapata vyakula na mazao ya biashara, hakutakuwa na njaa wala umaskini wa kipato na pia tutaishi kutokana na Kuvuta hewa safi.Usemi huo una mashiko ni vyema tukarithisha watoto wetu kuanzia wawapo shuleni ili waweze kutambua umuhimu wa kutunza mazingira"ameongeza Mhe. chana
Amesema ni muhimu klabu za mazingira zilizopo katika maeneo yetu kuendelea kuzisimamia ili zilete tija kwani kupitia klabu hizo wanafunzi watajifunza hifadhi ya mazingira, utalii na pia watajenga uelewa wa kutosha kutenda popote wawapo kwa falsafa ya "Jenga kesho iliyo bora (BBT)".
Amepongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa kuandaa Filamu ya Tanzania the Royal Tour na Amazing Tanzania ambapo amesema kuanzishwa kwa Tamasha la Utalii la Same ni kufuata maono ya Mhe. RAIS katika kutangaza utalii.
Akifafanua kuhusu faida ya Tamasha hilo amesema limesaidia kuwaletea wageni, pia kutoa elimu mbalimbali ya uhifadhi wa mazingira na utunzaji wa vyanzo vya maji kama misitu wa Chome.
Pia kuhusu kuboresha na Tamasha hilo, Mhe. Chana ametaka kuwepo na mikakati madhubuti ya kuendeleza Tamasha hilo kwa Halmashauri kutenga bajeti kuliko kuwaachia wadau wachache na uongozi wa Wilaya hiyo huku akisisitiza kuwa suala la uhifadhi na utalii lipo kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
"Ndugu zangu suala hili ni la msingi sana hata baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alisisitiza kuwa rasilimali hizi lazima zilindwe na ndiyo maana tuna Jeshi la Uhifadhi"amefafanua Waziri Chana
Ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na Serikali kuwabaini watu waovu, wanaotaka kuhujumu rasilimali za watanzania.
"Kuna changamoto za maingiliano tuliangalie ili wasilete madhara".
Mkuu wa Wilaya ya Same kaslida Mgeni amesema Tamasha la Same Utalii Festival limeonesha mafanikio makubwa ambapo hadi sasa wawekezaji watatu wamejitokeza na kuanza ujenzi wa hoteli kubwa za kisasa, Hoteli hizo zinajengwa katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, ikiwemo mbele ya Lango hifadhi ya Taifa ya Mkomazi na ndani ya hifadhi ya mazingira asilia Chome maarufu msitu wa Shengena
Kumeshuhudiwa pia ongezeko la wageni waliotembelea maeneo mbalimbali ambapo hifadhi ya taifa mkoamazi pekee kuna zaidi ya wageni 14,000 walitembelea hifadhi hiyo katika kipindi cha kuanzia Februari hadi Desemba yam waka huu 2024, ikilinganishwa na watu 7,000 kipindi kama hicho mwaka wa nyuma.
Aidha Dc Kasilda alieleza hayo wakati wa ufunguzi wa Msimu wa Pili wa Tamasha la Same Utalii Festival akitoa taarifa ya mafanikio tangu ilivyo adhimishwa msimu wa kwanza mwezi februari mwaka huu 2024 akisema mafanikio mengine ni Pamojana ajira kwa vijana na fursa za kibiashara kwa wajasiriamali wadogo.
“Mpaka sasa tumepata wawekezaji watatu kupitia tamasha lililopita, wameamua kujenga hoteli za hadhi katika wilaya yetu. Hoteli ya kwanza inajengwa mbele ya Lango kuu la kuingilia Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, nyingine inajengwa mbele ya hifadhi hiyo na nyingine inajengwa ndani ya msitu wa hifadhi ya mazingira asilia Chome na hoteli zote zina hadhi ya zaidi ya nyota mbili, jambo ambalo ni mafanikio makubwa kwa wilaya yetu,” alifafanua Kasilda Mgeni.
Malengo makuu ya tamasha hilo ni kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kutangaza sekta ya utalii ambapo tamasha hilo linatoa fursa kwa wakazi wa Same kunufaika na vivutio vya utalii vilivyo katika maeneo yao, kuwezesha ajira kwa vijana na kuvutia wawekezaji.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Metheusela Ntonda amesisitiza kuendelea kufungamanisha Utalii na utamaduni kwenye matamasha hayo.
Tamasha hilo limepambwa na wasanii mbalimbali na ambao watatoa Elimu na kuburudisha Kwa wageni wa ndani na Nje ya Tanzania
</
Post A Comment: