Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda, alipowasili katika viwanja vya Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano (AICC) Jijini Arusha, kwenye Kongamano la 15 la Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi nchini.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Dotto Biteko (wapili kushoto), Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) (watatu kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Arusha. Mhe. Paul Makonda (wakwanza kushoto), wakitembelea mabanda mbalimbali ya Maonesho katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano (AICC), kabla ya kufungua Kongamano la 15 la Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi nchini jijini Arusha.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande, akizungumza wakati akimkaribisha Mgeni Rasmi wa Kongamano la 15 la Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Dotto Biteko,, (hayupo pichani), kwa ajili ya kufungua Kongamano hilo lililofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano (AICC) jijini Arusha.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Dotto Biteko, akizungumza wakati akifungua Kongamano la 15 la Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi, lililofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano (AICC), alipokuwa Mgeni Rasmi katika Kongamano hilo.
Washiriki wa Kongamano la 15 la Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi, wakifuatilia matukio mbalimbali katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano Arusha (AICC), Kongamano hilo limehusisha viongozi na wadau mbalimbali pamoja na Wataalam wa Ununuzi na Ugavi, ambao wamesisitizwa kufanya kazi kwa uadilifu ili kukuza uchumi wa nchi.
Kamishna wa Sera za Ununuzi wa Umma na Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, katika Kongamano la 15 la wataalam wa ununuzi na ugavi, Dkt. Frederick Mwakibinga (wa kwanza kushoto), akiwa na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuziw a Umma (PPRA) Bw. Denis Simba, wakifuatilia Kongamano hilo katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano Arusha (AICC) jijini Arusha.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Dotto Biteko, (katikati walioketi), akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) (wapili kushoto, walioketi), Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda (wakwanza kushoto, walioketi) pamoja na viongozi wengine na washiriki wa Kongamano la 15 la wataalam wa ununuzi na ugavi jijini Arusha.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (wakwanza kushoto), akiagana na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano (AICC) Bi. Chritine Mwakatobe, baada ya Ufunguzi wa Kongamano la 15 la Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi lililofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano Arusha (AICC).


Na. Ramadhani Kissimba na Asia Singano, WF - Arusha


Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo mbalimbali inayosimamia kada ya Ununuzi na Ugavi nchini.

Akizungumza katika ufunguzi wa kongamano la 15 la Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi nchini linalofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano (AICC) Jijini Arusha, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, amewataka Wataalamu hao kuzitendea haki taaluma zao kwa kufanya kazi kwa uadilifu ili kuhakikisha sekta ya ununuzi na ugavi inawatoa watu kwenye umasikini.

Mhe. Dkt. Biteko alisema kuwa Sekta ya Ununuzi na Ugavi ndio eneo pekee linalochukua takribani asilimia 70 ya Bajeti ya Serikali, hivyo uadilifu pekee ndio utakaosaidia fedha kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa hasa katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.  

Aidha, Dkt. Biteko aliwaasa Wataalamu hao kuzingatia na kuyaishi yale yaliyopo kwenye sheria za manunuzi kwa kufanya kazi yenye tija, uwazi na kujiepusha na vitendo vya rushwa kwenye masuala yote ya manunuzi ya Umma.

‘’Serikali iliamua kuanzisha sheria ya manunuzi ili kuwa na manunuzi yenye tija, kupata bidhaa zenye ubora na wakati, na kuondoa mianya ya rushwa., hivyo naomba mkutano huu uzingatie yale yanayotafsiriwa kwenye sheria hiyo’’alisema Mhe. Dkt. Biteko.

Mhe Biteko aliipongeza Bodi ya Usimamizi wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), kwa hatua mbalimbali inazochukua hasa kwa wale wanaoenda kinyume na maadili ya sekta hiyo na kusisitiza kuwa Serikali kupitia bodi hiyo haitasita kuwachukulia hatua kali watumishi ambao watashindwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria zilizopo.

Awali akimkaribisha Naibu Waziri Mkuu, Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alisema kuwa Wizara ya Fedha imeendelea kuwapa thamani na kutoa kipaumbele kwa wataalamu wa ununuzi na ugavi ili kuhakikisha wanafanya vizuri katika eneo lao la kazi ili kukuza uchumi.

‘’Kupitia Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura 410 tumewapa hadhi ya kuwa Wakurugenzi, Mameneja n.k kwa kuzingatia ukubwa wa Taasisi nunuzi na hivi sasa, Wizara inaendelea na jitihada za kurekebisha Muundo wa Vitengo vya Ununuzi na Ugavi ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi’’ alisema Mhe. Chande.

Kongamano la Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi ambalo lilikuwa na kauli mbiu ya Mabadiliko ya Ununuzi na Ugavi kwa Usimamizi Bora wa Rasilimali linafanyika kila mwaka kwa lengo la kutoa fursa kwa Bodi ya Usimamizi wa Ununuzi na Ugavi kukutana na wataalamu wake pamoja na wadau wa mnyororo wa ununuzi na ugavi, ili kujadiliana kwa pamoja jinsi ya kuboresha utendaji kazi katika mnyororo mzima wa ununuzi nchini.
Share To:

Post A Comment: