Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka amekemea ongezeko la matukio ya ukatili wa kijinsia na mauaji katika baadhi ya maeneo ya Mkoa huo kwa mwaka 2024 ikiwemo suala la udumavu
Aidha vitendo vya ukatili ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu vinavyosababishwa na majeraha makubwa ya kimwili na kisaikolojia kwa waathirika.
Kwamujibu wa waraka wake kwenda kwa jamii ikiwemo viongozi wa dini, Mtaka amesema vitendo hivyo kiujumla vinafedhehesha taswira nzuri ya mkoa huo na vinastahili kulaaniwa kwa nguvu zote na wananjombe kwamba si utamaduni wala mila zao na si Utaifa na wala si utanzania na ni vitendo visivyo beba sura halisi ya Mungu.
Amesema ofisi ya Mkuu wa Mkoa inalaani vikali matukio haya na kusisitiza kuwa matukio haya ya kikatili hayana nafasi ndani ya Mkoa na ndani ya jamii yetu tutahakikisha tunapambana na matukio haya kwa nguvu zote kama Serikali hakikisha tunayakomesha ili kutengeneza jamii ya wananjombe.
"Tunaomba waraka huu usomwe kwenye nyumba zote za ibada zitakazofanya Misa au ibada ya siku ya Sikukuu ya Krismasi Tarehe 25 Desemba, 2024 na siku ya Mwaka Mpya tareahe 1 Januari, 2025, pia waraka huu usomwe kwenye nyumba za Ibada siku ya Ijumaa tarehe 3 Januari 2025, tarehe 4 Januari, 2025 na tarehe 5 Januari, 2025."
Ndugu Wananchi wa Mkoa wa Njombe, Tunapokaribia Msimu wa Sikukuu ya Krismasi na kuanza Mwaka Mpya 2025, ningependa kutumia fursa hii kuzungumzia masuala mawili muhimu yanayogusa mustakabali wa Mkoa wetu, mosi kutokomeza udumavu na kupinga ukatili wa kijinsia na mauaji.
UDUMAVU
Takwimu na taarifa za Serikali Kitaifa zinaonyesha Mkoa wa Njombe una kiwango kikubwa cha Udumavu (asilimia 50.4%) kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano kwa mujibu wa Utafiti wa Afya, Demografia na Viashiria vya Malaria wa Mwaka 2022.
Hali inayosikitisha na inayohitaji juhudi za dhati kutoka kwetu sote,Udumavu una athari kubwa kwenye ukuaji wa mwili na akili ya mtoto hivyo huchangia maendeleo duni shuleni, uwezo mdogo wa kufikiri, kujifunza na ubunifu.
Kwa watu wazima udumavu huchangia kuwa na uwezo mdogo wa uzalishaji mali, ambapo kulingana na viwango vya Shirika la Afya Duniani (WHO), kiwango cha udumavu cha kuanzia asilimia 20 kinachukuliwa kuwa ni cha juu hivyo kuhitaji juhudi za makusudi za kukipunguza.
Katika juhudi za kupunguza/kutokomeza udumavu, Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama UNICEF, TFNC, USAID mradi wa Lishe na wadau wengine imekuwa kwenye kampeni Maalum ya kuongeza kasi ya kupunguza/kutokomeza Udumavu yenye jina "LISHE YA MWANAO, MAFANIKIO YAKE inayochagizwa na Kaulimbiu isemayo KUJAZA TUMBO SI LISHE, JALI UNACHOMLISHA".
Kampeni hii inabeba uzito mkubwa kutokana na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye kwa nyakati tofauti amezungumzia tatizo la udumavu kwa Mkoa wa Njombe na kutoa maelekezo mahususi kwa viongozi wa Mkoa wa Njombe na Wilaya zake kuchukua hatua za kuhakikisha tatizo la Udumavu linapungua kwa kiasi kikubwa/linatokomezwa.
Katika kampeni hii mambo yafuatayo yanahimizwa na kupewa msukumo mkubwa ambapo matumizi ya vyakula mchanganyiko kwa watoto kutoka katika makundi sita ya vyakula kulingana na
mwongozo wa chakula na ulaji Tanzania Bara kama vile vyakula vya nafaka, mizizi yenye wanga, ndizi mbichi, vyakula vya asili ya wanyama, vyakula vya jamii ya mikunde, kokwa na mbegu za mafuta, mbogamboga, matunda na mafuta yenye asili ya mimea ambayo ni salama kwa afya.
Pili,Elimu kwa akina mama kuhusu umuhimu wa lishe bora wakati wa ujauzito na kunyonyesha.
Tatu, Ufuatiliaji wa ukuaji na maendeleo ya watoto kupitia vituo vya kutolea huduma za afya na ngazi ya jamii ili kuhakikisha wanapokea huduma stahiki za Afya na Lishe.
Kwa Pamoja kama jamii, wazazi na walezi, tuhakikishe kila mtoto anapata nafasi ya kukua vizuri na kufikia ndoto zake.
Ni jukumu letu sote kupambana na tatizo la udumavu katika familia zetu kwani uwezo tunao tukiwa ni Mkoa ambao Mungu ametupa neema ya mvua na ardhi nzuri inayozalisha vyakula vyote vinavyohusika na lishe bora.
Malengo ya Mkoa ifikapo mwaka 2030 tatizo la Udumavu liwe katika kiwango kinachohimilika kulingana na vigezo viliyo salama tukiamini NJOMBE BILA UKATILI WA KIJINSIA NA MAUAJI INAWEZEKANA.
Serikali ya Mkoa inawataka na kuwaomba wananchi mambo yafuatayo:
Mosi, Wananchi kutoa taarifa za vitendo vya ukatili mapema kupitia vyombo vya usalama, namba zifuatazo
zinaweza kutumika kutoa taarifa kwa NAMBA YA POLISI 119, TAKUKURU 113, namba ya kutoa taarifa za Ukatili Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Njombe ni 0738 68 24 34.
Pili, Viongozi wa Kisiasa, Madhehebu ya dini, mila na makundi mengine katika jamii kushiriki kikamilifu kuelimisha wananchi kuondokana na Imani za kishirikina, visasi, tamaa za mali na madaraka na kuendelea kuelimisha jamii kuhusu athari za ukatili wa kijinsia na mauaji.
Sambamba na haya, Idara ya Afya ndani ya Mkoa kushiriki kuelimisha wananchi kuhusu changamoto na matatizo ya Afya ya akili lakini pia jamii inakumbushwa wajibu wa wazazi/ walezi malezi bora ya familiayanayozingatia imani ya dini na desturi nzuri zinazomjenga mtoto kuwa Mwananjombe/Mtanzania mzalendo na mwenye maadili mazuri.
Pia Vyombo vya dola kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wale wote wanaohusika au kubainika na vitendo hivi na haki ionekane.
Napenda kusisitiza kwamba vyombo vyetu vya utoaji haki vitakuwa msaada mkubwa kwa waathirika na wahanga wote watakao thibitika kushiriki matendo haya ya fedheha na yanayo tweza utu wa binadamu, Serikali itaendelea kuhakikisha usalama wa kila mwananchi, jambo kubwa wananchi watoe ushirikiano wa taarifa kwenye Ofisi za Serikali ngazi za Vitongoji, Vijiji, Mitaa, Kata, Tarafa, Wilaya na Mkoa Pamoja na namba ambazo zimeoneshwa kwenye taarifa hii.
HITIMISHO
Ndugu wananchi, naomba mpokee pole nyingi sana kutoka Ofisi ya Mkoa kwa wanafamilia wote ambao matukio ya ukatili wa kijinsia na mauaji yamewagusa kwa namna moja ama nyingine nirudie dhamira yangu na viongozi wenzangu ndani ya Mkoa yakuona mambo haya ya ovyo hayajirudii tena ndani ya Mkoa wetu.
Tushirikiane kwa dhati kuhakikisha tunatokomeza udumavu, na tuzingatie umuhimu wa lishe bora kwa watoto wetu na kwasisi watu wazima tuzingatie mlo ulio bora, ufanyaji wa mazoezi ili kuondokana na changamoto kubwa ya sasa ya magonjwa yasiyo ambukiza kama vile kisukari, shinikizo la juu la damu, magonjwa ya moyo, figo na baadhi ya saratani.
Ni Imani yangu kwamba kwa Pamoja tutaishinda vita hii,
Mungu ibariki Njombe,Mungu ibariki Tanzania, Kheri ya Krismasi na Kheri ya Mwaka Mpya 2025
Ni mimi Mtumishi wenu
Anthony Mtaka
Mkuu wa Mkoa wa Njombe
Post A Comment: