Wahitimu wa chuo cha uhasibu arusha wapatao 5854, wamekumbushwa kutumia tafiti zao walizozifanya wakiwa chuo ili ziweze kusaidia jamii na taifa kwa ujumla.
Akizungumza katika mahafali ya 26 ya mwaka 2024 Naibu waziri wa fedha (mb) Hamad Hssan Chande, amewataka kutumia changamoto walizokutana nazo na kuzifanya njia ya kufikia mafanikio wanayoyatarajia
"Nawapongeza sana kwa hatua hii, lakini mkiaminiwa jiaminishe, mkawe na subira na kujifunza kuridhika, kuwa wavumilivu na kuacha tamaa ya kuharakia maisha, naamini mkizingatia haya mtafanikiwa na kutimiza ndoto zenu"
" Sasa tanueni wigo wa taaluma zenu, kama mlivyotembelea SADC, fungueni matawi huko nina imani mtakubaliwa, na hatua hii itaongeza kiwango cha wanafunzi ili kufikia lengo" amekumbusha Chande
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Cha Uhasibu Arusha profesa Eliamani Sedoyeka, amewatakia wanafunzi wote waliohitimu kozi mbalimbali heri na fanaka tele katika maisha yao baada ya kumaliza masomo, ambapo jumla ya wahitimu 5854 kati yao wanaume ni 3601 na wanawake 2253 kwa ngazi ya astashahada, stashahada, shahada na shahada za uzamili katika fani mbalimbali.
Hata hivyo amewaasa wahitimu kuendelea kujituma, kutochagua kazi na kushirikiana na kila mmoja katika jamii ili kuendelea kujifunza mambo muhimu ya kujijenga na kuzingatia nidhamu ya pesa na muda.
Katika namna hiyo ameishukuru serikali kwa kuwapatia kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 40 kupitia mradi wa elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi (HEET), kwamba kupitia fedha hizo wanatarajia kujenga songea, na baadhi ya majengo katika kampasi ya babati na arusha yakiwemo madarasa, maabara za kompyuta, jengo la utawala na kituo cha umahiri cha TEHAMA, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuendelea kuboresha na kuweka mazingira rafiki ya kujifunzia.
"Tumefanikiwa kutoa wahitimu wa kwanza katika kozi tatu za shahada na kozi moja ya shahada ya uzamili, kozi hizo za shahada ni shahada ya usalama wa mtandao, Shahada ya Uanagenzi katika usimamizi wa utalii na ukarimu, na shahada katika menejimenti ya maktaba na taarifa, kozi hizi tatu za shahada zilianza rasmi mwaka wa masomo 2020/2021" amefafanua profesa Sedoyeka.
"Kipekee nimefurahi kuona mmefikia hatua hii kubwa, ni imani yangu mtazidi kufanikiwa iwapo mtazingatia yale yote mliyoelekezwa na walimu wenu, nawakaribisha tena hapa chuoni kuongeza kiwango cha elimu sisi tuko tayari kuwatumikia na nitawakumbuka sana" ameeleza Profesa Sadoyeka.
Mwenyekiti wa baraza la uongozi wa chuo cha uhasibu Arusha Dkt. Mwamini Tulli, amesema chuo kimeweka mpango mkakati wa kuongeza idadi wanafunzi wanaojiunga na chuo hicho, mikakati hiyo inaendana na ujenzi wa majengo mapya yanayokidhi vigezo vya watu wenye ulemavu na wale wasiokuwa na changamoto pamoja na ukarabati wa miundombinu mingine.
"Mimi kama mama nasikia furaha kubwa kuona idadi ya wanawake wanaohitimu leo ni kubwa kiasi hiki, nawasihi mkatumie vizuri taaluma zenu ili mkalete mabadiliko katika jamii zenu, mzidi kuaminika na kuwafanya wazazi wenu kujivunia" amesema Tulli.
Mwakilishi wa wanafunzi aliyehitimu elimu ya shahada ya kwanza katika chuo hicho, na Rais wa wanafunzi mstaafu Shafii Rajab ameushukuru uongozi wa chuo hicho, walimu na walezi kwa kuwasaidia na kuhakikisha leo wanatimiza ndoto yao ya kumaliza masomo.
"Kipekee nawapongeza wazazi wetu kwa kuamini katika kuwasomesha watoto wa kike, nafurahi maana ukisomesha mtoto wa kike umeikomboa jamii, lakini pia wazazi wetu mmefanya kazi kubwa ya kutulipia ada na kutushauri ndio maana leo tuko hapa tunafurahia matunda ya kujitoa kwenu",
"Tunaahidi tutaenda kufanyia kazi kile tulichokipata, kwa maana ya kuwa wabunifu, kujituma, uadilifu na kuchangamkia fulsa zilizoko mtaani, nasema tumepikwa na tumeiva kutokana na elimu hii, hivyo tunategemea kujenga uchumi wetu na taifa kwa ujumla" amesema Shafii.
Post A Comment: