Na Munir Shemweta, WANMM

 

Wadau wa sekta ya milki mkoa wa Dar es Salaam na Pwani  wametoa maoni mbalimbali kuhusiana na utambuzi na Usajili wa wadau wa sekta ya milki nchini.

 

Mjadala kuhusu Utambuzi na Usajili wa wadau wa sekta ya milki umefanyika jijini Dar es Salaama jana na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo wadau kutoka Chama cha Wamiliki wa Ardhi na Nyumba Tanzania, Umoja wa Makampuni yanayomiliki na kuuza viwanja Dar es Salaama na Pwani, Chama cha Wapangaji na Wapangishaji pamoja na Umoja wa Wataalamu wa Milki tanzania (AREPTA).

 

Wakizungumza wakati wa kutoa maoni kuhusiana mjadala huo, wadau wa milki wamesema, ipo haja kwa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kushirikiana na wadau ili kuifanya sekta ya milki kufanya kazi kwa ufanisi.

 

"Tunataka tuungane maana sisi siyo washindani, tuungane katika kufanya kazi zetu" amesema Emilian Rwejuma, Mwenyekiti wa Umoja wa Makampuni yanayomiliki na kuuza viwanja Dar es Salaam na Pwani.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wapangaji na Wapangishaji Bw. Abdallah Msangama amesema, maisha yamekuwa hatarishi kutokana na migogoro mbalimbali kama vile migogoro ya upangaji inayojitokeza huku akisisitiza makazi bora ni yale yasiyokuwa na migogoro.

 

Aidha, amegusia suala la utoaji elimu kwa wapangaji na kusema kuwa, serikali kwa sasa  inakosa fedha nyingi kupitia masuala ya kodi na kusisitiza utoaji elimu kwa wenye nyumba na wapangaji ili kuelimika na kuepuka changamoto ndogo ndogo alizozieleza kuwa  hazina maana.

 

"Niishukuru Wizara ya Ardhi kwa kuleta maono ya mjadala wa sekta ya milki ya namna tunavyokwenda katika kuiboresha sekta hii"amesema

 

Rais wa Wataalamu wa Milki Tanzania (AREPTA) Andrew Kato amesema, kumekuwa na changamoto kadhaa katika tasnia ya milki jambo linaloifanya sekta hiyo kutoheshimika ambapo ametaka sekta hiyo iheshimike kama ilivyo kwenye nchi nyingine.

 

Amesema, ni vizuri pakawepo utaratibu mzuri wa upangishaji nyumba tofauti na ilivyo sasa ambapo hakuna utaratibu maalum jambo alilolieleza linalosababisha madalali kuchukua fedha kutoka kwa wapangaji, wanunzi, wauzaji na wenye nyumba

 

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Kitengo cha Milki Wizara ya Ardhi Nyunba na Maendeleo ya Makazi Bw. Wilson Wairara amesema, wizara ya Ardhi haihitaji kumtenga mtu yeyote katika suala la milki bali kuweka utaratibu mzuri unaoweza kuchochea weledi na ufanisi katika kufanya shughuli zake.

 

Akielezea maono na malengo ya wizara katika kukuza sekta ya milki nchini amesema, kwa sasa suala la kanzidata kwa wadau wa milki linatiliwa mkazo kwa kuwa kama idadi ya wadau haijulikani itakuwa ni changamoto hata kufanya mipango madhubuti ya kuisukuma sekta ya milki. 

 

"Tunakwenda kuleta mfumo mzuri utakaoweza kusaidia katika kukusanya taarifa mbalimbali zikiwemo za makampuni kitu ambacho ni muhimu sana". amesema

 

Ameongeza kwa kusema, Wizara ya Ardhi haitaweza kufanya kazi zake bila ushirika mkubwa wa wadau wa sekta ya milki hivyo msisitizo wake ni kushirikiana na wadau katika kuiboresha au kurahisisha utekelezaji wa shughuli za sekta milki.

 

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Kitengo cha Milki (Real Estate) inaendesha mijadala ya pamoja na wadau kwa lengo la kupata maoni kuhusu utambuzi na usajili wa Wadau wa Sekta ya Milki ili kuboresha na kukuza sekta ya milki nchini.

 

Share To:

Post A Comment: