Katika kusherehekea SIkukuu za Krismasi na Mwaka Mpya 2025, Watanzania hatuna budi kujivunia safari ya mafanikio katika Sekta ya Nishati, hususan umeme.
Je Unajua kabla ya kupata Uhuru mwaka 1961 Nchi ilizalisha umeme kwa kutumia mafuta ambapo kila mkoa ulijitegemea na hapakuwepo na mfumo wa gridi ya Taifa?
Safari ya Mabadiliko (yaani Journey of Transformation) ilianza mwaka 1967 kwa ujenzi wa kituo cha kuzalishaji umeme cha Hale megawati chenye uwezo wa megawati 21 pamoja na ujenzi wa njia ya umeme kutoka Hale hadi Dar es Salaam na hivyo kuanza kwa mfumo wa gridi ya Taifa.
Kutokana na nishati ya umeme kuwa ndio kichocheo cha ukuaji wa uchumi, utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme iliendelea ambapo mwaka 1968 ulifanyika ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme cha Nyumba ya Mungu cha megawati 8, mwaka 1975 kikajengwa Kituo cha Kidatu cha megawati 204 pamoja na ujenzi wa njia ya umeme ya Kidatu – Morogoro – Dar es Salaam.
Safari ya Mabadiliko iliendelea kufanyika kupitia Viongozi Wakuu wa Nchi wa awamu mbalimbali ambao walipelekea ujenzi wa vituo vya umeme vya Mtera ( 80MW) mwaka 1988 na ujenzi wa njia ya umeme ya Mtera – Iringa, Mtera – Dodoma na hivyo kuongeza mtandao wa gridi ya Taifa.
Vikafuata vituo vya kuzalisha umeme vya New Pangani Falls (68MW) mwaka 1995, na ujenzi wa vituo vya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia vya Songas (189MW) mwaka 2006, Tegeta Gas Engine (45MW) mwaka 2009, Ubungo I (102MW) mwaka 2008, Ubungo II (129MW) mwaka 2012 na Ubungo III (92.5MW) mwaka 2012, Kinyerezi I (335MW) mwaka 2023 na Kinyerezi II (248.2MW) mwaka 2018.
Kazi haijaishia hapo kwani utekelezaji miradi ya umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali inaendelea, mfano halisi ni mradi wa JNHPP ambao sasa unazalisha zaidi ya megawati 1000 pamoja na mradi wa Rusumo unaoipatia Tanzania megawati 26.667.
Pamoja na kuzalisha umeme wa kutosha, Serikali kupitia Wizara ya Nishati inaendelea kuimarisha mfumo wa gridi ya taifa ili kuhakikisha nchi nzima inafikiwa na mtandao wa gridi ya taifa na hivyo kuzidi kuimarisha upatikanaji wa umeme nchini.
TUNAJIVUNIA hatua hii kubwa iliyopigwa katika Sekta ya Nishati.
Heri ya Krismasi na Mwaka Mpya 2025.
Post A Comment: