Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango, ameiagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuandaa mpango maalum wa kukabiliana na matukio ya moto katika misitu ya asili na mashamba ya miti, kama sehemu ya juhudi za kulinda rasilimali za misitu nchini. 

Hii ni pamoja na kuanzisha kampeni za uhamasishaji kwa jamii kuhusu umuhimu wa misitu, ufugaji nyuki, na jinsi ya kushiriki katika shughuli za urejeshaji wa uoto wa asili.

Agizo hilo lilitolewa Disemba 11,2024 na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dustan Kitandula, kwa niaba ya Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango, wakati wa uzinduzi wa Kongamano la Tatu la Kimataifa la Kisayansi lililozinduliwa jijini Arusha. 

Kongamano hili lenye kauli mbiu “Kurejesha Mandhari ya Misitu kwa Maendeleo Endelevu na Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchi” lilihusisha wataalamu zaidi ya 900 kutoka ndani na nje ya nchi.

Aidha, Kitandula alisisitiza umuhimu wa TAFORI kushirikiana na taasisi nyingine za utafiti ili kuja na suluhisho za kudhibiti mimea vamizi katika hifadhi za misitu nchini. 

Alizitaka taasisi hizo kuzungumza na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia taasisi zake pamoja na Mfuko wa Misitu Tanzania kutenga fedha kwa ajili ya tafiti zitakazosaidia kutatua changamoto zinazokabili sekta ya misitu, nyuki, na mazingira.

Aliongeza kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii inatakiwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali, sekta binafsi, na serikali za mitaa ili kuunda mikakati ya pamoja ya urejeshaji misitu. 

Aidha, alisisitiza kutoa mafunzo kwa wakulima na jamii kuhusu mbinu za kilimo endelevu, ufugaji nyuki, na uhifadhi wa misitu.

Pia, alisisitiza umuhimu wa kuboresha miundombinu kwenye maeneo ya mashamba ya miti na kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya mazao ya misitu na nyuki ili kuhamasisha uzalishaji bora wa mazao hayo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TAFORI, Prof. Verdiana Masanja, aliiomba serikali kutenga fedha kwa ajili ya shughuli za utafiti ambazo zitatoa majibu sahihi kwa changamoto zinazozikumba sekta hizo. 

Alielezea changamoto za uhaba wa wataalamu, miundombinu chakavu ya maabara, na upungufu wa wataalam wa misitu, ambapo alisema Tanzania ina wataalamu wa misitu 85 tu nchini kote

Mjumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Lucy Mayenga, alisema sekta ya misitu ni muhimu kwa uchumi wa taifa na inalinda mazingira, ikichangia katika uhifadhi wa vyanzo vya maji na usawa wa kiikolojia kwa wanyama na mimea. 

Aliongeza kuwa, licha ya umuhimu wake, sekta hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa za ongezeko la idadi ya watu na shughuli za kibinadamu katika maeneo ya misitu. 

Alisisitiza kuwa wabunge wataendelea kuishauri serikali kutenga fedha kwa ajili ya TAFORI ili kujiendesha na kutoa motisha kwa wataalamu wa sekta hiyo.








Share To:

Post A Comment: