Na Benny Mwaipaja, Oman


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Kisultan ya Oman, zimetia saini Mkataba wa Kuondoa Utozaji Kodi ya Mapato Mara Mbili na Kuzuia Ukwepaji Kodi, ujulikanao kama Agreement for the Elimination of Double Taxation with Respect to Taxes on Income and Prevention of Tax Avoidance and Evasion.

Mkataba huo umesainiwa Mjini Mascut nchini Oman na Waziri wa Fedha wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mapato ya Oman, Bw. Nasser Al-Jashmi.

Mhe. Dkt. Nchemba amesema kuwa kusainiwa kwa mkataba huo ni hatua muhimu katika jitihada za Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, za kufungua uchumi wa nchi kwa kuvutia uwekezaji wa kimataifa.

Ameongeza kuwa Mkataba huo utawezesha wawekezaji na wafanyabiashara wanaofanya shughuli kati ya Tanzania na Oman kutozwa kodi mara moja pekee, badala ya kutozwa mara mbili kwa mapato ya aina moja, hali ambayo awali ilikuwa ikikwaza ustawi wa biashara kwa pande zote mbili.

Mkataba huo pia unalenga kuvutia mitaji mikubwa kutoka Oman kuja kuwekeza Tanzania, hususan kupitia kampuni kubwa zinazomilikiwa na familia za kifalme, sambamba na wawekezaji binafsi ambapo kupitia uwekezaji huo, Tanzania inatarajia kunufaika na ukuaji wa sekta za uzalishaji, maendeleo ya viwanda, na kuongezeka kwa ajira kwa wananchi.

Aidha, wawekezaji wa Kitanzania sasa wataweza kuwekeza Oman bila vizuizi vya kikodi, huku wakilindwa na mkataba huo ili kuepusha kulipishwa kodi mara mbili.

Hatua hiyo pia inatoa fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania kupanua shughuli zao katika masoko ya kimataifa, hasa katika ukanda wa Ghuba.

Kwa ujumla, Mheshimiwa Dkt. Nchemba amesema kuwa mkataba huo unatarajiwa kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Oman, huku Oman ikivutiwa zaidi na fursa za uwekezaji nchini Tanzania kutokana na jiografia yake ya kimkakati, vivutio vyake vya kiuchumi, na mazingira bora ya uwekezaji ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), akisaini kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mkataba wa Kuondoa Utozaji Kodi ya Mapato Mara Mbili na Kuzuia Ukwepaji Kodi, ujulikanao kama An Agreement for the Elimination of Double Taxation with Respect to Taxes on Income and Prevention of Tax Avoidance and Evasion. na Serikali ya Kisultan ya Oman, ikiwakilishwa na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mapato ya Oman, Bw. Nasser Al-Jashmi. Tukio hilo limefanyika Makao Makuu ya Mamlaka ya Kodi, Mjini Muscat nchini Oman na kushuhudiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Sheria, Wizara ya Fedha-Tanzania, Bw. Elias Kalist na kwa upande wa Oman, alikuwepo Mtaalam wa masuala ya Uhusiano wa Kimataifa, Bi. Salwa Khalfan Eid-Al-salti. Mhe. Waziri Dkt. Nchemba yuko katika ziara ya kikazi nchini Oman.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), akibadilishana Hati ya Mkataba na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mapato ya Oman, Bw. Nasser Al-Jashmi. Mkataba unaohusu makubaliano ya Kuondoa Utozaji Kodi ya Mapato Mara Mbili na Kuzuia Ukwepaji Kodi, ujulikanao kama An Agreement for the Elimination of Double Taxation with Respect to Taxes on Income and Prevention of Tax Avoidance and Evasion. Kati ya Tanzania na Serikali ya Kisultan ya Oman, Tukio hilo limefanyika Makao Makuu ya Mamlaka ya Kodi, Mjini Muscat nchini Oman, ambapo Mhe. Waziri Dkt. Nchemba yuko katika ziara ya kikazi nchini humo.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mapato ya Oman, Bw. Nasser Khamis Al-Jashmir, wakionesha Hati ya Mkataba unaohusu makubaliano ya Kuondoa Utozaji Kodi ya Mapato Mara Mbili na Kuzuia Ukwepaji Kodi, ujulikanao kama An Agreement for the Elimination of Double Taxation with Respect to Taxes on Income and Prevention of Tax Avoidance and Evasion. Kati ya Tanzania na Serikali ya Kisultan ya Oman. Tukio hilo limefanyika Makao Makuu ya Mamlaka ya Kodi, Mjini Muscat nchini Oman, ambapo Mhe. Waziri Dkt. Nchemba yuko katika ziara ya kikazi nchini humo.
Share To:

Post A Comment: