Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) imefungua rasmi mafunzo ya siku tano kwa wataalamu wa mashine za mionzi zinazotumika katika hospitali mbalimbali nchini kwa lengo la kuwajengea uwezo katika utendaji wao wa kazi wa kuwahudumia wananchi.
Akifungua mafunzo hayo Jijini Arusha katika ofisi za TAEC Kanda ya Kaskazini Mkurugenzi wa udhibiti na usimamizi wa mionzi (TAEC) DKT. JUSTIN NGAILE amesema mafunzo hayo ni muhimu sana na yanajumuisha wataalamu 60 wanaotumia mashine za X ray, C T Scan na MRI ambapo mafunzo hayo yatawasaidia kuhakikisha wao wanakuwa salama wanapotumia mashine hizo pamoja na wateja wanaowahudumia.
Aidha DKT. NGAILE ameongeza kuwa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania ndiyo mdhibiti wa matumizi ya mionzi nchini na kuwataka wote wenye mashine za mionzi kuhakikisha wanazingatia sheria na taratibu za matumizi ya vyanzo vya mionzi ili kujihakikishia usalama.
Kwa upande wake Mkufunzi wa Chuo cha afya Muhimbili idara ya mionzi anayehudhuria mafunzo hayo Bi CATHERINE MALIKA amesema mafunzo yanayotolewa na TAEC yanawasaidia kuwaimarisha katika kazi zao za kila siku za kuwahudumia wananchi.
Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) imejiwekea utaratibu wa kutoa mafunzo kwa wataalamu wa mashine za mionzi nchini ili kuhakikisha wafanyakazi wa mashine hizo wanakuwa salama, wateja wao pamoja na mazingira.
Post A Comment: