Serikali ya Tanzania imesema itaendelea kuwa mstari wa mbele kupigania usawa katika masuala ya kazi kwa watu wote bila kujali hali zao ikiwemo kuhimiza uwepo wa kazi zenye staha na kupinga ubaguzi dhidi ya watu wenye ulemavu.


Kauli hiyo ya serikali imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, wakati akifunga mafunzo ya Usalama, Afya, Haki na Wajibu kwa watu wenye ulemavu yaliyoandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kwakushirikiana na Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi.

Mafunzo hayo yaliyojumuisha washiriki zaidi ya 100 yamewahusisha watumishi wa Mahakama na Taasisi nyingine za umma ambao wana ulemavu mbalimbali na yamefanyika katika Ukumbi wa OSHA Dodoma kwa siku mbili mfulizo (Desemba 16-17, 2024).

Katika hotuba yake Waziri Kikwete amesema: “Mkataba Na. 159 wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) unahimiza usawa katika masuala ya kazi kwa watu wote bila kujali wana ulemavu au la kwani takwimu zinaonesha 15% ya watu wote duniani ni wenye ulemavu na moja ya changamoto za kundi hili ni kufanyishwa kazi zisisokuwa na staha na kubaguliwa. Hivyo, Tanzania kama mwanachama wa ILO itaendelea kuhimiza utendaji wa kazi zenye staha na kupinga vikali ubaguzi dhidi ya watu wenye ulemavu,” ameeleza Waziri Kikwete.

Aidha, amesema mafunzo yanayotolewa na OSHA ni utekelezaji wa wajibu wa serikali wa kulinda nguvukazi yake kupitia usimamizi wa Sheria Na.5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 ambapo ameitaka OSHA kuendelea kutekeleza wajibu huo ipasavyo kwa makundi mbalimbali katika jamii.

Awali akifungua mafunzo hayo Desemba 16, 2024, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Tanzania, Dkt. Mustapher Siyani aliipongeza OSHA na Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi kwakuona umuhimu wa kuandaa mafunzo hayo maalum ambayo yamekuwa ni nadra sana kutolewa kwa watumishi wa serikali.

“Pamoja na kwamba serikali imekuwa ikitoa mafunzo mbalimbali kwa watumishi wake kwa ujumla lakini ni aghalabu sana kuwa na mafunzo maalum kama haya yanayojumuisha watumishi wenye ulemavu mbalimbali tena wanaotoka katika kanda zote ndani ya nchi yetu. Hongereni sana waandaaji wa mafunzo haya kwa kuona umuhimu wa mafunzo haya,” ameeleza Jaji Kiongozi.

Aidha, amewaasa washiriki wa mafunzo kutumia vizuri fursa waliyoipata kwa niaba ya wenzao wengi ambao wamebaki katika vituo vya kazi kwa kushiriki kikamilifu na kuhakikisha kwamba wanajifunza mambo mapya ambayo yatasaidia kuboresha mazingira yao ya kazi na kuleta tija katika utendaji wa Taasisi wanazotoka.

Kwa upande wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi, Dkt. Yose Mlyambina, ameeleza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha walengwa kushiriki katika mapambano dhidi ya magonjwa, ajali, vifo na madhira mengine yanayotokea mahali pa kazi pamoja na kutambua haki na wajibu wao katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Akitoa salama zake katika ufunguzi wa mafunzo husika, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, ameeleza sababu za OSHA kushirikiana na Mahakama kuwa ni utekelezaji wa maagizo ya Serikali ya Awamu Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, inayotaka mifumo ya serikali kusomana.

“OSHA ni wasimamizi wa Sheria Na.5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 na chombo pekee chenye wajibu wa kutafsiri sheria ni Mahakama hivyo ni muhimu kwa Taasisi hizi mbili kufanya kazi kwa pamoja”, ameeleza Kiongozi Mkuu wa Taasisi ya OSHA.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete, akihutubia katika hafla ya kufunga mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi ambayo yametolewa kwa watumishi wa Mahakama ya Tanzania na Taasisi nyingine za watu wenye ulemavu yaliyo fanyika katika Ofisi za OSHA Jijini Dodoma Disemba 17, 2024.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi.Khadija Mwenda, akizungumza kwenye hafla ya kufunga mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi, ambayo yametolewa kwa watumishi wa Mahakama ya Tanzania na Taasisi nyingine za watu wenye ulemavu yaliyo fanyika katika Ofisi za OSHA Jijini Dodoma Disemba 17, 2024.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu- Divisheni ya Kazi, Dkt. Yose Mlyambina, akitoa salamu zake katika hafla ya kufungua mafunzo ya usalama na afya pamoja haki na wajibu wa wafanyakazi kwa watumishi wa Mahakama na Taasisi nyingine ambao wana ulemavu mbalimbali.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Tanzania, Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, akifungua mafunzo maalum ya usalama na afya pamoja na haki na wajibu kwa watumishi wa Mahakama na Taasisi nyingine ambao wana ulemavu mbalimbali.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na Amos Rweikiza, Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni ambaye alishiriki mafunzo ya afya, usalama, haki na wajibu wa wafanyakazi mahali pa kazi katika hafla ya kufunga mafunzo hayo.
  Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda na Kamishna wa Kazi, Bi. Suzan Mkangwa na wakifuatilia hafla ya kufunga mafunzo ya usalama na afya pamoja haki na wajibu wa wafanyakazi kwa watumishi wa Mahakama na Taasisi nyingine ambao wana ulemavu mbalimbali.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete na meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu wa Mahakama mbalimbali nchini kwenye hafla ya kufunga mafunzo ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania na Taasisi nyingine za watu wenye ulemavu yaliyo fanyika katika Ofisi za OSHA Jijini Dodoma Disemba 17, 2024.

Watumishi wa Mahakama ya Tanzania na watumishi wa Taasisi nyingine za watu wenye ulemavu wakiwa kwenye mafunzo ya usalama, afya, haki na wajibu wa wafanyakazi mahali pa kazi yaliyo fanyika katika Ofisi za OSHA Jijini Dodoma Disemba 17, 2024.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Tanzania, Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (Katikati) na meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa OSHA mara baada ya kufungua mafunzo ya usalama na afya pamoja na haki na wajibu kwa wafanyakazi wenye ulemavu mahali pa kazi.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Tanzania, Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (Katikati) pamoja na viongozi wengine wa meza kuu wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya usalama na afya pamoja na haki na wajibu kwa wafanyakazi wenye ulemavu mahali pa kazi, Desemba 16, 2024.
Share To:

Post A Comment: