Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wameendesha mafunzo maalum kwa
watu wenye ulemavu katika Wilaya ya Bukombe, Mkoa wa Geita, kwa lengo la
kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na kugawa majiko ya gesi yenye
mitungi ya kilo 6.
Waliofaidika na mpango huu ni jumla ya watu 64 wenye mahitaji
maalum, wakiwemo wasioona, wenye ualbino, na wenye usikivu hafifu. Mafunzo haya
yamefanyika sambamba na kampeni ya serikali ya kuhakikisha makundi yote katika
jamii yanapata fursa ya kutumia nishati safi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Katibu Tawala wa Wilaya
hiyo, Ally Mketo, ameishukuru REA kwa kuendesha mafunzo hayo na kusisitiza
umuhimu wa matumizi sahihi ya nishati safi ili kuboresha maisha na afya ya
walengwa.
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi Tanzania (TAMAVITA), Kelvin Nyema, pamoja na Mwenyekiti wa Wasioona Wilaya ya Bukombe, Rosemary Nuhu, wameelezea manufaa waliyopata kutokana na mafunzo hayo. Wamepongeza juhudi za REA katika kuhakikisha watu wenye ulemavu wanajengewa uwezo wa kutumia nishati salama na rafiki wa mazingira.
Mpango huu wa REA ni sehemu ya dhamira ya serikali ya
kuhakikisha wananchi wote, wakiwemo wenye mahitaji maalum, wanapata nishati
salama na endelevu.
Post A Comment: