Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuanzia tarehe 20 Januari, 2025 itaanza kusambaza mitungi ya gesi ya kilo 6 mkoani Manyara ili kusaidia wananchi kutumia nishati hiyo kwa ajili ya kupikia.

Hayo yamesemwa, tarehe 16 Desemba, 2024 na Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Teknolojia Mbadala, kutoka REA, Mhandisi, Advera Mwijage mbele ya Queen Sendika, Mkuu wa mkoa wa Manyara, ofisini kwake, Babati, mkoani humo.

Katika mpango huo, mkoa wa Manyara unatarajia kupokea mitungi ya gesi 16,275 yenye thamani ya shilingi milioni 284 ambayo, itasambazwa kwa wananchi katika wilaya zote tano huku kampuni ya MANJIS Logistic Ltd ikipewa jukumu la kusambaza mitungi hiyo kwa gharama ya shilingi 17,500 kwa kila mtungi (Bei ya ruzuku).

Imeelezwa kuwa Serikali, itatoa ruzuku ya asilimia 50 kwenye kila mitungi ambapo bei ya awali, ilipaswa kuwa shilingi 35,000 ili kununua mtungi pamoja na kichomeo chake.

RC Sendiga, amepongeza juhudi hizo za Serikali na kuongeza kuwa lengo la Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia ni kuwa ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia, jambo ambalo litasaidia kutunza na kuhifadhi mazingira.

“Serikali, imeweka ruzuku ya asilimia 50, kwa hiyo wakina baba na kina mama wa mkoa wa Manyara, wajiandae kutumia gesi, tuwapunguzie wakina mama kushika masizi, kutumia kuni na mikaa, kwetu sisi mradi huu ni neema”. Amesema Sendiga.

Kwa upande wake, Mhandisi, Adivera Kaijage amesema kwa nchi nzima mradi huo wa kusambaza mitungi ya gesi ya kilo 6 kwa wananchi utagharimu shilingi bilioni 8 ambapo kwa mkoa wa Manyara shilingi milioni 284 zitatumika kugharamia mitungi 16,275.

“Kampuni ya MANJIS imeshinda, tenda ya kusambaza mitungi hiyo, ilitangaza ofa ya kusambaza mtungi mmoja kwa shilingi 35,000 kwa kutambua hilo, Serikali italipia asilimia 50 ya bei hiyo, ambayo itakuwa shilingi 17,500.” Amefafanua, Mhandisi, Advera.

Mhandisi, Advera amesema ili kupata mtungi huo wenye ruzuku ya Serikali kila mwananchi anapaswa kuwa na kitambulisho cha NIDA au namba ya NIDA.

Amesema, REA pia, inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali, ambapo ametoa taarifa ya mradi wa mkopo wenye riba nafuu kwa ajili ya ujenzi wa vituo vidogo vya mafuta katika maeneo ya vijijini huku akisema watu wengi wamekuwa wakitunza mafuta katika nyumba wanazoishi jambo ambalo ni hatari kiafya pamoja na ubora wa mafuta hayo.

“Tumeona vyombo vya moto vya watu wa vijijini vitaharibika kwa sababu mafuta wanayotumia ni machafu, hayana uhifadhi mzuri unaohitajika, lakini pia gharama za usafiri maeneo ya vijijini ni kubwa na wananchi hawanufaiki kwa bei elekezi zinazotolewa na serikali”. Amesema Mhandisi, Advera na kuongeza,

“Mkopo huo utalipwa ndani ya miaka 7; kwa riba ya asilimia 5; mkopo hauzidi milion 133, kwa ajili ya kujenga kituo ambacho kutakuwa na matenki mawili yenye ujazo wa lita 15,000”.

Mhandisi Kaijage pia ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Manyara kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu kwa ajili ya maombi ya mkopo nafuu wa ujenzi wa vituo vidogo vya mafuta maeneo ya vijijini.

Mkoa wa Manyara una jumla ya wilaya 5; wilaya hizo ambazo wananchi wake watanufaika na mitungi ya gesi ni Babati, Hanang, Simanjiro, Mbulu na Kiteto.

Share To:

Post A Comment: