Mkuu wa mkoa wa Njombe Antony Mtaka ameonyesha kusikitishwa na matukio ya mauaji na ukatili ambayo yanaripotiwa katika mkoa wake huku akitaka jamii kutambua kuwa kila mmoja anawajibu wa kudumia usalama kwa kuripoti kwenye vyombo vya ulinzi na usalama pindi aonapo viashiria vya uhalifu.
Aidha Mtaka amekemea kitendo cha baadhi ya wananchi kujichukulia sheria mkononi na kueleza kuwa hali hiyo inakiuka misingi ya utawala bora na vina athari kubwa katika maendeleo ya jamii.
Akizungumza katika kikao cha dharura ambacho kimehusisha viongozi wa kimila,viongozi wa Dini na wawakilishi kutoka taasisi na makundi mbalimbali katika jamii ili kujadili na kushauriana kuhusu wimbi la vitendo vya ukatili wa kijinsia yakiwemo mauaji na ubakaji ambao umeendelea kujitokeza katika mkoa huu unaotajwa kukua kwa kasi kiuchumi, Mtaka amesema haiwezekani kila kukicha matukio ya aibu,unyama yanatokea na kuchafua mkoa wa Njombe hivyo kikao hicho kitoke na majibu ili kunusuru maisha ya watu.
Akieleza mwenendo wa matukio kwa kipindi cha miaka mitano Kamanda wa Polisi mkoa wa Njombe ASP Mahamoud Banga amesema takribani matukio 366 ya mauaji yametokea kuanzia mwaka 2020 hadi 2024 ,unyang'anyi wa kutumia siraha yakiwa 16,unyang'anyi wa kutumia nguvu 48,ubakaji 829 huku ulawiti yakiwa matukio 91 na kueleza kwamba uchunguzi wa matukio mengi umebaini wanaotenda matukio ni watu jirani ama ndugu.
Wakitoa ushauri na maependekezo nini kifanyike kudhibit matukio hayo ,wawakilishi wa makundi mbalimbali katika jamii wakiwemo viongozi wa mila,viongozi wa dini na tiba asili wamesema ziundwe kamati zitakazopita kijiji kwa kijiji kutoa elimu kwasababu kuna tatizo kubwa la afya ya akili ,visasi na tamaa ya mali.
Post A Comment: