Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa mchango wa shilingi milioni 35 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Kanisa la Agrican lililopo mjini Makambako. Mchango huo umewasilishwa na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, akimwakilisha Rais Samia, katika hafla iliyofanyika leo kanisani hapo.

Akizungumza kwa niaba ya Mhe. Rais, Mhe. Mtaka amesema kuwa Rais Samia amewapongeza viongozi wa dini kwa juhudi kubwa wanazofanya katika kusaidia maendeleo ya kijamii, ikiwemo kusimamia maadili na kuwaongoza waumini kuwa raia wema. "Madhehebu ya dini na viongozi wa kidini mnafanya kazi kubwa sana ya kusaidia maendeleo ya nchi yetu. Endeleeni kuliombea mema taifa letu na kusimamia maadili kwa waumini wenu," amesema Mhe. Mtaka kwa niaba ya Rais.

Aidha, Mhe. Rais kupitia Mhe. Mtaka ametoa wito kwa viongozi wa dini kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wa Mkoa wa Njombe kuhusu umuhimu wa kuepuka tabia ya kujichukulia sheria mkononi, kitendo kinachopelekea mauaji na ukatili wa kijinsia. Pia, amesisitiza umuhimu wa kuhimiza lishe bora ili kutokomeza tatizo la udumavu linaloikumba mkoa huo.

Zaidi ya shilingi milioni 60 zimepatikana kupitia hafla hiyo, ambapo wachangiaji wengine wameungana na Mhe. Rais kuchangia tukio hilo. Mchango huo umeleta matumaini makubwa kwa waumini wa Kanisa la Agrican Makambako.

Akitoa shukrani, Askofu wa Kanisa hilo, Mhe. Matthew Mhagama, amesema, "Tunamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kuwa Mgeni Rasmi kwenye hafla hii kupitia mwakilishi wake na kwa mchango wake wa shilingi milioni 35. Pia, tunawashukuru viongozi wote walioshiriki katika hafla hii na kuchangia, kufanikisha jumla ya zaidi ya shilingi milioni 60. Mchango huu utasaidia sana kukamilisha ujenzi wa kanisa letu."

Hafla hiyo imehitimishwa kwa dua ya shukrani, huku waumini wakionyesha furaha na shukrani kwa jitihada za pamoja katika kufanikisha maendeleo ya kiroho na kijamii.






Share To:

Post A Comment: