Naibu Waziri wa Madini,Dkt Steven Kiruswa amemaliza mgogoro wa muda mrefu kati ya Kampuni ya Madini ya Paradiso unaomilikiwa na Victor Mkenga Maarufu kwa jina la Jangu Master unaochimba madini ya Rubby katika Kata ya Mundarara Wilayani Longido Mkoani Arusha na Lukumay Malulu (90) baada ya Kampuni hiyo kuamua kumilipa fidia ya shilingi milioni 150 Mzee huyo ili aweze kuachi ardhi yenye migodi hiyo.
Kiruswa awali kabla ya kuanza vikao kwa kusikilza pande zote mbili alisema kuwa mgogoro huo ni wa zaidi ya miaka nane na aliwataka wenye mgogoro kuacha kurumbana pasipo sababu kwani Wizara ya Madini kwa sasa inataka kufunga mwaka kwa kuhakikisha migogoro yote nchini inakwisha na kuanza mwaka ujao kwa mambo mengine yenye kuiletea nchi maendeleo.
Alisema Kampuni ya Paradiso inamiliki migodi kihalali ikiwa ni pamoja na Wizara ya Madini kutoa lesseni ya uchimbaji Madini ya Rubby kwa Kampuni hiyo na Mzee Malulu anamiliki ardhi ya migodi hiyo na serikali ya Kijiji inamtambua hilo.
Waziri Kiruswa alisema Serikali haiwezi kuzivuta au kumnyang'anya Paradiso Lesseni ilitoa yenyewe kwa kuwa Kampuni hiyo haijavunja masharti yoyote katika uchimbaji na Serikali inamtambua Mzee Malulu kama mmiliki halali wa ardhi iliyopo migodi ya Paradiso.
Alisema Mkuu wa polisi Wilaya ya Longido {OCD} Richard Matagi na Kaimu Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Arusha,Bi.Bertha Luzabiko na kamati yake wamefanya kazi kubwa ikiwa ni pamoja na kukutana na pande zote na kujua kwa kina chanzo cha mgogoro hatima ya mgogoro huo na kuja na suluhushi la kampuni ya Paradiso kumlipa fidia Mzee Malulu cha shilingi milioni 150 kwa kuwa alikaa hapo kwa muda mrefu na alikuwa na uhusiano mzuri na marehemu mzee Philipo Mkenga mzazi Victor.
Kiruswa alisema uamuzi wa Paradiso unapaswa kupongezwa kwani ni uamuzi wenye busara na hekima na alimshauri Mzee Malulu kukubaliana na hilo kwani tathimini ya kiserikali ikifanyika kiwango kinachotakiwa kupata kutoka kwa Paradiso kinaweza kupungua kwa asilimia kubwa hivyo akubali kuchukua kiasi hicho cha fedha na mzee Malulu alikubaliana na hilo.
Waziri kiruswa mbali ya kuwa na watendaji wa Wizara kutoka Dodoma katika kutatua mgogoro huo pia alikuwa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali Wilaya ya Longido akiwemo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi{CCM}Wilaya ya Longido,Papa Mollel,Diwani wa Kata ya Mundarara,Alex Ruben,Viongozi wa Vijiji na Viongozi wa Jumuiya zote za Chama Longido na Kamati yote ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Longido na kusema Serikali kwa sasa haitaki migogoro migodini.
''Ninaiomba Kampuni ya Raradiso kuhakikisha januari 30 mwakani wawe wameshamlipa Mzee Malulu shilingi milioni 100 na kiasi kingine kimalizwe kabla ya kuisha mwezi march mwakani''alisema Kiruswa
Mzee Malulu na mwanae Joseph Malulu waliitaka Kampuni ya Paradiso kuhakikisha inatimiza ahadi yake katika muda uliopangwa bila kuwa na ubabaishaji wowote lengo ni kutaka familia ya Mzee Malulu na Kampuni hiyo kuwa kitu kimoja.
Walimshukuru sana Waziri Kiruswa kwa kumaliza mgogoro huo uliowafanya kuhangaika kule na huko bila mafanikio na kusema kuwa hiyo imewafanya kuwa na imani ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwa ana watendaji wanaopenda haki na kupinga vita dhuruma kitu ambachio sio sawa.
Mzee Malulu alimshukuru OCD Matagi na kamati yake kwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha mgogoro huo unamalizika kwa amani na hilo limefanikiwa na alisema amewapa baraka wakurugenzi wa Kampuni ya Paradiso katika shughuli zao kwa kuwa ana amani na hana tena kinyongo na wao.
Naye Meneja wa Kampuni ya Paradiso,Samwely Msangi akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Paradiso,Victor Mkenga kwanza alimshukuru Waziri Kiruswa kwa kusimamia mgogoro huo na kufikia mwisho na pili aliishukuru fanmilia ya Mzee Malulu kwa kukubali kwa moyo mmoja kumalizika kwa mgogoro huo kwa kulipwa kiasi hicho cha fedha.
Msangi alisema wana muda mrefu hawajazalisha madini katika migodi yao na kutokana na kumalizika kwa mgogoro huo huenda mambo yakawa mazuri na kampuni itakuwa na ushirikiano wa hali na mali kwa familia ya mzee Malulu na serikali ya Kijiji lengo ni kutaka kuwa na mahusiano mazuri yenye tija.
Naye Kaimu Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Arusha,Bertha Luzabiko alisema mgogoro huo ulikuwa ukimsumbua sana kwani muda wake mwingi alikuwa akitumia katika vikao mbalimbali vya pande hizo mbili na kufikia mwisho hiyo imempa faraja na kuona sasa Arusha mpya katika sekta ya migodi imeibuka.
Post A Comment: