Na Mapuli Kitina Misalaba

Mashindano ya Krismas Cup yanayoendelea katika Kijiji cha Salawe, Wilaya ya Shinyanga Vijijini, yamezidi kuonyesha ushindani mkubwa baada ya mechi ya leo kati ya Machongo FC na Mwabenda FC kumalizika kwa matokeo ya kusisimua.

Mechi hiyo imeanza kwa kasi huku Junior wa Machongo FC akifunga bao la kwanza dakika ya 14 na kuipa timu yake uongozi wa mapema. Hata hivyo, Mwabenda FC imesawazisha kupitia penalti iliyofungwa na Sylvester dakika ya 45, na kufanya mchezo huo kumalizika kwa sare ya 1-1 ndani ya dakika 90.

Baada ya sare hiyo, mshindi ameamuliwa kwa mikwaju ya penalti ambapo Mwabenda FC imeibuka kidedea kwa ushindi wa penalti 4-2, hivyo kusonga mbele katika mashindano haya yenye ushindani mkubwa.

Mgeni rasmi wa mechi ya Disemba 1, 2024 ni Afisa Mifugo wa Kata ya Salawe, Gasper Ronald Makawa, ambaye amempongeza mwandaaji wa ligi hiyo Bwana Makamba Lamecki, kwa juhudi zake za kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana na kwamba amewasihi wachezaji kutumia mashindano hayo kama fursa ya kufikia ndoto zao katika michezo.

Viongozi wengine waliotoa pongezi ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Songambele, Lazaro Enock Lazaro, Mtendaji wa Kijiji cha Songambele, Evalina Isack, na Afisa Maendeleo wa Kata ya Salawe Emmy Kwayu pamoja na mambo mengine wamesema ligi hiyo ni msaada mkubwa kwa vijana na ni tukio linaloleta mshikamano miongoni mwa wananchi, hasa kwa kuwa mashindano hayo ni bure kwa wananchi wote.

Msimamizi wa Ligi ya Krismas Cup, Mwalimu Emmanuel Enock Kijida, ametoa taarifa ya mechi inayofuata.
"Disemba 2, 2024 kutakuwa na mechi kati ya Salawe FC na Solwa FC, kwa hiyo atakayeshinda mechi ya kesho ndiye atakayekutana na mshindi wa mechi ya leo, ambaye ni Mwabenda FC. Nawakaribisha sana wananchi wote kuja kuburudika, kwani hii mechi ni ya derby." Amesema Mwalimu Kijida

Mashindano haya yanatarajiwa kufikia kilele tarehe 17 Disemba 2024, kwa fainali itakayofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mhangu, Kijiji cha Songambele ambapo Mfumo wa mtoano utaendelea kutumika hadi hatua ya mwisho.

Ligi hii, iliyoandaliwa na Makamba Mussa Lameck kupitia kampuni yake ya MCL inayojihusisha na biashara ya nafaka, imelenga kuibua vipaji vya michezo katika Mkoa wa Shinyanga huku ikileta mshikamano wa kijamii.

Kwa habari zaidi kuhusu mashindano haya na matukio mengine ya michezo, endelea kufuatilia MISALABA MEDIA.

Mgeni rasmi wa mechi ya  Disemba 1, 2024 ni Afisa Mifugo wa Kata ya Salawe, Gasper Ronald Makawa, akimpongeza Makamba Lameck kwa kuandaa ligi ya michezo bila wananchi kutoa hela.

Mgeni rasmi wa mechi ya  Disemba 1, 2024 ni Afisa Mifugo wa Kata ya Salawe, Gasper Ronald Makawa, akimpongeza Makamba Lameck kwa kuandaa ligi ya michezo bila wananchi kutoa hela.

Msimamizi wa Ligi ya Krismas Cup, Mwalimu Emmanuel Enock Kijida, akitoa taarifa ya mechi inayofuata.


Share To:

Misalaba

Post A Comment: