Na Denis Chambi, Tanga.

KATIKA kuendelea kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuunga mkono Serikali juu ya mpango wa matumizi ya nishati safi shirika la World Vision kupitia mradi wake wa Ardhi Tanga Project  limekuja na mpango wa kurejesha uoto wa asili  katika maeneo yaliyoharibiwa kutokana na shughuli za kijamii ikiwemo uvunaji  wa miti  usio rasmi pamoja na uchomaji wa mkaa.

Hayo yameelezwa na meneja wa Mradi huo  Benson Mseli katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wenyeviti wa vijiji, watendaji pamoja na maafisa Misitu waliopo katika wilaya za Pangani, Mkinga ,Handeni na Kilindi kwaajili ya kwenda kutekeleza mradi huo ambapo ameeleza kuwa wamebaini zaidi ya asilimia 60 ya maeneo ya Misitu yameharibiwa.

"Ni dhahiri kwamba hatuwezi tukaishi bila ya kutengemea rasilimali za Misitu  lakini ni namna gani ambavyo tunavuna kwa namna endelevu  ambazo haziwezi kuathiri  kizazi cha sasa na kijacho mradi wa Ardhi Tanga  Project tunatoa wito  kwa jamii waweze kutunza hifadhi za Misitu tunataka kurejesha uoto wa asili pamoja na ile miti ya kupandwa  katika maeneo yetu"

"Katika tathmini tulizozifanya World Vision tumegundua kuwa zaidi ya asilimia 60 ya maeneo ya Misitu yameharibiwa  kwahiyo tunatamani ule uharibufu ambao ulifanyika  usiendelee kuwepo ,sisi kama mradi wa Ardhi tumejikita  katika vijiji 40 ya mkoa wa Tanga katika wilaya 4 tuna lengo la kufikia watu zaidi ya elfu 20 katika yao asilimia 60 ni vijana tunaamini wana nguvu na ndio Taifa la leo na kesho" alisema Mseli.

Alisema World Vision inaungana na Serikali katika mapango wake wa 2030 katika kuhakikisha jamii ya watanzania inabadilika na kuhama kutoka kwenye matumizi ya nishati chafu kwenda kwenye nishati safi.

" Sisi kama World Vision Tanzania na mradi wa Ardhi tunaungana na Serikali kuhakikisha kwamba baada ya miaka 10 angalau zaidi ya asilimia 80 ya kaya za watanzania  watakuwa wanatumia nishati safi ya kupikia tutaendelea kusisitiza matumizi ya Kuni chache, majiko bunifu ili kuhakikisha kwamba tunapunguza matumizi ya nishati zinazotokana na Misitu ili tuweze kutunza mazingira yetu" alisema Mseli.

Meneja huyo amebainisha kuwa kundi la wanawake wamekuwa ni waathirika wa moja kwa moja kutokana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuiangalia shilo shirika la World Vision limejipanga kuwawezesha nishati endelevu ya kupikia na hatimaye kuondokana na matumizi ya Kuni na mkaa.

"Sisi kama World Vision kwa ufadhili wa ulaya tumeweza kuona mabadiliko ya tabianchi kumekuwa ni janga na hakuna hakuna jambo ambalo tunaweza kulifanya zaidi ya uhifadhi wa Misitu yetu Kuna ongezeko la uharibufu wa mazingira ukiangalia kwa mwaka  2018 uharibufu umefikia asilimia 80 hali sio nzuri"

" Wanawake ndio waathirika wakubwa wa  mabadiliko ya tabianchi  hivyo kwa kulitazama hili tutakuwa na kundi la  wanawake asilimia 60 ambao  tutawasaidia waweze kuanzishwa mashamba ya miti kwaajili ya Kuni lakini mwisho wa siku tuweze kuungana na Serikali kuhakikisha  wanaweza kupatiwa namna ambayo watatumia nishati endelevu" alisema.

Akizungumza katika mafunzo hayo yaliyofanyika kwa siku mbili katibu tawala msaidizi Mkoa wa Tanga katika  sekta ya uzalishaji  Emigidius Kasunzu amewataka wenyeviti wa kamati za utunzaji wa mazingira , mafisa  Misitu pamoja na watendaji wa kata na vijiji  waliopo katika wilaya zinazoguswa na mradi huo hususani Handeni na Mkinga kuhakikisha wanashirikiana kupiga vita biashara ya mkaa ambayo inaendelea kwa sasa hali ya kuwa Serikali inaelekeza  wananchi kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi.

"Sisi sote tuna jukumu la kuhimiza matumizi ya nishati safi tuhakikishe kuwa hakuna uvunaji wa Misitu holela sasa hivi ukiangalia kwenye wilaya zetu hususani Handeni na Mkinga kuna wimbo kubwa sana la uvunaji wa Mkaa na viongozi tupo tukishuhudia hilo linafanyika  tubadilishe fikra zetu badala ya kuwa na mawazo ya kuchoma mkaa  twende mawazo ya kuhakikisha kwamba tunatunza na kupanda miti kuliko kuendelea na biashara hii ambayo tunapata fedha kidogo kutokana na kuchoma mkaa"

Aidha amewataka kuendelea kutekeleza  agizo lililotolewa na Mkoa  kuanzishwa vitalu vya miche ambayo watapaswa kuigawa Bure kwa wananchi kwaajili ya kupanda kwenye maeneo mbalimbali ili kurudisha uoto wa asili katika maeneo ambayo yanahitajika kupandwa miti.

"Niendelew kuwasisitiza kuanzishwa vitalu vya miche twende tukaa ili mwisho wa siku tuhakikishe hiyo miche tunaigawa kwa wananchi ili waweze kushiriki kwenye hii kampeni ya kurejesha uoto, tuhakikishe kwamba kabla hatujavuna tunakuwa na miti ya kutosha iliyopandwa ni jukumu letu sisi sote" amesisitiza Kasunzu.

Baadhi ya watendaji , wenyeviti na maafisa Misitu wa wilaya zinazoguswa na mradi huo wameahidi kwenda kutekeleza  mpango wa urejeshaji wa Misitu kwa kuwashirikisha wananchi ili kutimiza adhima ya shirika hilo pamoja na Serikali katika kuhamasisha jamii kutunza mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yanayoweza kujitokeza.

Share To:

Post A Comment: