Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Geita (GEREFA) leo kimefanya uchaguzi wake mkuu ambapo aliyekuwa Mwenyekiti wa GEREFA Mkoa wa Geita, Salum Kulunge, amepitishwa bila kupingwa kuendelea na nafasi hiyo. Wajumbe wa Kamati Tendaji waliochaguliwa ni Domisian Kabalega Butula na Kassim Mustapha Nangale.
Kwa upande wa nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa, uchaguzi ulizua ushindani mkali kati ya wagombea watatu: Ally Ismail Twist, Leonard Mnenge Suluja, na Simon Joseph Shija. Suluja alipata kura sifuri, huku Twist na Shija wakigongana mara mbili kwa kura nane kila mmoja. Kutokana na hali hiyo, Mwenyekiti wa uchaguzi, Mwanasheria Kwandu Mapalala, alitangaza kuwa uchaguzi wa nafasi hiyo utafanyika tena ndani ya siku 60.
Akizungumza wakati wa mkutano huo, Salum Kulunge aliwashukuru wajumbe kwa kuonyesha imani kubwa kwake na kueleza kwa kina namna mchakato wa uchaguzi ulivyoendeshwa kwa uwazi kupitia kamati tendaji.
“Ninawashukuru wajumbe wote kwa kuniamini kuendelea kuongoza chama hiki. Tutashirikiana kwa pamoja kuhakikisha maendeleo ya soka mkoani Geita yanaimarika.” Salum Kulunge – Mwenyekiti wa GEREFA Mkoa wa Geita:
Kwa upande wake, Mgeni Rasmi wa shughuli hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe Paskasi Muragili, amewataka wagombea na wajumbe kuchukulia uchaguzi huu kama sehemu ya demokrasia na sio uwanja wa uhasama.
“Uchaguzi ni sehemu ya kutekeleza demokrasia. Ni muhimu kushindana kwa haki na mshikamano bila kujenga uhasama wa aina yoyote.” Paskasi Muragili - Mkuu wa Wilaya ya Bukombe:
Mwenyekiti wa uchaguzi, Mwanasheria Kwandu Mapalala, pia alisisitiza kwamba mchakato wa uchaguzi ulifuata misingi ya uwazi na haki, huku akiwataka wajumbe wote kushiriki kwa amani katika uchaguzi wa marudio.
Uongozi mpya wa GEREFA unatarajiwa kuendeleza juhudi za kuboresha mpira wa miguu mkoani Geita, hasa kwa kuwapa nafasi vijana wenye vipaji kuonyesha uwezo wao kupitia ligi na mashindano mbalimbali. Wajumbe waliopitishwa wamesisitizwa kushirikiana kwa karibu ili kutekeleza mikakati ya maendeleo ya soka na kujenga mshikamano ndani ya chama.
Aidha, uchaguzi wa marudio kwa nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa unatarajiwa kuwa wa haki na uwazi kwa mujibu wa mwongozo uliowekwa na GEREFA.
Post A Comment: