Na Mapuli Kitina Misalaba
Timu ya Salawe Stars imeibuka washindi wa mashindano ya Krismas Cup 2024, yaliyomalizika leo Desemba 19, 2024 kwa fainali kali dhidi ya Beya FC na kwamba ligi hiyo imeandaliwa na Makamba Mussa Lameck kwa lengo la kuibua vipaji vya michezo.
Katika mchezo huo ambao umechezwa kwa dakika 90 bila kufungana, Salawe Stars walitawazwa mabingwa baada ya kushinda mikwaju ya penati 5-4, na kujinyakulia kombe pamoja na zawadi ya Shilingi milioni moja.
Mshindi wa pili, Beya FC, wamezoa zawadi ya Shilingi laki tano, huku Mwasenge FC wakishika nafasi ya tatu na kupata Shilingi laki mbili.
Wachezaji bora, mfungaji bora, kipa bora, na timu yenye nidhamu pia walitunukiwa zawadi za fedha, kutambua mchango wao kwenye mashindano hayo.
Mgeni rasmi wa fainali hizo, Diwani wa Kata ya Salawe, Mhe. Joseph Buyugu, ameipongeza Salawe Stars kwa ushindi huo na kuwaomba wadau wa michezo kumuiga Makamba Mussa Lameck ili kuandaa mashindano zaidi.
“Michezo si tu afya, bali pia ni njia ya kujenga upendo na mshikamano. Nawashauri timu zilizoshiriki ziendelee kujifunza. Natamani kuona ligi kama hizi zinaendelea ili kuibua vipaji na kuimarisha michezo wilayani Shinyanga,” amesema Buyugu.
Mdhamini wa mashindano hayo, Makamba Mussa Lameck, ameipongeza jamii kwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia michezo ambapo amekanusha uvumi kuwa mashindano hayo yalihusiana na siasa, akisisitiza kuwa lengo lake kuu ni kuibua vipaji vya michezo kwa vijana.
“Mashindano haya hayakuhusiana na siasa. Ni jitihada za kuibua vipaji na kuwapa vijana wetu fursa ya kushiriki mashindano makubwa. Nawahakikishia mashindano haya yataendelea kila mwaka,” amesema Makamba.
Pamoja na changamoto za kisiasa zilizojaribu kukwamisha ligi hiyo, Makamba ameishukuru serikali ya kijiji kwa kusimama imara kuhakikisha mashindano hayo yanafanikiwa.
Kwa mujibu wa msimamizi wa mashindano hayo, Mwalimu Emmanuel Enock Kijida, vijana 50 kati ya timu 16 zilizoshiriki mashindano hayo wamechaguliwa kuunda timu moja itakayoshiriki mashindano mbalimbali.
Mashindano ya Krismas Cup 2024 yamedhaminiwa na Makamba Mussa Lameck kupitia kampuni ya MCL, inayojihusisha na biashara ya nafaka, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuchochea maendeleo ya michezo mkoani Shinyanga.
Post A Comment: