Kila wilaya kupata majiko 3,255 Kilimanjaro wamshukuru Rais Samia
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unatarajia kusambaza jumla ya majiko ya gesi (LPG) ya kilo sita 19,530 yanayotolewa kwa bei ya ruzuku ya 50% Mkoani Kilimanjaro ikiwa ni utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034.
Hayo yameelezwa Novemba 6, 2024 na Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji Miradi REA, Mhandisi Emanuel Yesaya Mkoani Kilimanjaro wakati wa kutambulisha mradi wa kusambaza majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku sambamba na kumtambulisha msambazaji ambaye ni Kampuni ya Lake Gas katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.
"Tumeanza utekelezaji wa mradi wa kusambaza majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku tupo hapa kutambulisha rasmi mradi huu unaogharimu kiasi cha shilingi 407 kwa mkoa huu na pia kumtambulisha msambazaji katika mkoa huu ambaye ni Kampuni ya Lake Gas," amesema Mhandisi Yesaya.
Mhandisi Yesaya amesema REA imejipanga kutekeleza azma ya Serikali inayoongozwa na Rais. Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha ifikapo mwaka 2034; 80% ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.
Akizungumza wakati wa kupokea mradi huo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kiseo Nzowa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, aliipongeza REA kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kutekeleza dhamira na ajenda kuu ya Rais. Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.
"Tunashuhudia REA inatekeleza kwa vitendo dhamira ya Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wanatumia nishati safi kupikia na wanaachana na matumizi ya kuni na mkaa ili kulinda kuhifadhi mazingira na pia kulinda afya," amesema.
Ametoa wito kwa wananchi mkoani humo kuchangamkia fursa hiyo iliyotolewa na Serikali kupitia REA hasa ikizingatiwa kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia yanaokoa gharama na muda ambao mwananchi anaweza kutumia kufanya shughuli nyingine za kiuchumi lakini pia ni rafiki wa mazingira na afya kwa mtumiaji.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi kwa ujumla, Mhandisi Yesaya amesema kwa mwaka huu wa fedha 2024/2025, jumla ya majiko ya gesi 452,445 ya kilo sita yenye thamani ya shilingi bilioni 10 yatasambazwa kote nchini kwa bei ya ruzuku ya asimilia 50.
Mhandisi Yesaya ameeleza kuwa mbali ya mradi huo wa usambazaji wa majiko ya gesi; REA vilevile inaandaa mradi wa kusambaza majiko banifu kwa bei ya ruzuku ambapo alisema jumla ya majiko 200,000 yatasambazwa kwa bei ya ruzuku ya 75% hadi 85% kwa maeneo ya vijijini kote nchini.
Amesema lengo ni kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa kulingana na hali yake ya kiuchumi ili kufikia lengo kuu la mkakati la kufikisha 80% ya watanzania watakaotumia nishati safi na iloyo bora ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Post A Comment: