Wilaya ya Longido imehitimisha siku ya pili ya mafunzo ya uandikishaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura kwa wasimamizi wasaidizi ngazi ya kata. Mafunzo haya yameandaliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa lengo la kuwawezesha wasimamizi hao kutekeleza majukumu yao kwa umakini na weledi.

Akifunga mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Bw. Nassoro Shemzigwa, alitoa wito kwa washiriki kutunza vifaa watakavyokabidhiwa na Tume, akisisitiza kuwa vifaa hivyo ni muhimu kwa kufanikisha zoezi hilo. "Tutunze vifaa hivi kama mali ya taifa, na zaidi, tufanye kazi kwa kufuata sheria na taratibu tulizoelekezwa. Lengo letu ni kuhakikisha kila mwananchi mwenye sifa anapata nafasi ya kujiandikisha," alisema Shemzigwa.

Aidha, Mwenyekiti wa mafunzo hayo, Bw. Terevaeli Mbise aliipongeza Tume Huru ya Uchaguzi kwa juhudi zake za kuhakikisha mafunzo haya yanafanyika kwa kiwango cha juu. “Mafunzo haya ni muhimu sana kwa wasimamizi wa ngazi ya kata. Tumejifunza mengi na tunaahidi kuyatekeleza kwa ufanisi wa hali ya juu ili kuhakikisha kila mkazi wa kata husika anashiriki kikamilifu katika zoezi hili muhimu,” alisema.

Kwa upande wake, Afisa mwandikishaji  ngazi ya jimbo Bw Nevilling Lymo aliwashukuru washiriki kwa bidii waliyoonyesha katika mafunzo hayo. Alisema kuwa juhudi walizoweka ni ishara ya dhamira yao ya kuhakikisha zoezi linafanikiwa. "Napenda kuwapongeza kwa kujifunza kwa moyo wote. Maarifa haya ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha uboreshaji wa daftari unafanyika kwa usahihi na uwazi," aliongeza. 

Washiriki wa mafunzo hayo walieleza kuridhishwa na mafunzo waliyopokea, wakisema kuwa yamewaongezea maarifa muhimu ya kutekeleza majukumu yao kwa umakini mkubwa.

Mafunzo haya ni sehemu ya maandalizi ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura, hatua muhimu kuelekea chaguzi zijazo. Hii ni juhudi ya kuhakikisha kuwa demokrasia ya nchi inaimarika kwa kuwapa wananchi fursa ya kushiriki kikamilifu katika maamuzi ya kitaifa.


















Share To:

Post A Comment: