Baraza la Madiwani Jijini Arusha wamechachamaa wakihoji kwa nini miradi ya ujenzi wa barabara na uwekaji wa mitaro imeshindikana kukamilika hadi mvua zimeanza kunyesha, hatua inayopelekea madiwani kutoaminika kwa wananchi wao.
Wameibua hoja hiyo katika kikao cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/2025, wakihoji juu ya fedha zilizotengwa milioni 28 kwa kila kata kutengeneza miundombinu hiyo, na kutaka majibu yenye ufafanuzi kutoka kwa mwenyekiti wa baraza juu ya jambo hilo ambalo linawakosesha imani na wananchi wao.
Diwani wa viti maalum Sakina Mpanju, Isaya Doita wa Ngarenaro, Labora Ndarpoi waTemi, Naboth Silasie wa Lemala ni baadhi ya madiwani waliotaka ufafanuzi kwa nini miradi ya barabara imeshindikana kukamilika kwa wakati ilihali pesa zimeshatengwa.
"Sisi ndio tunaona adha wanayopitia wananchi, kama kipindi hiki mvua zinavyoendelea kunyesha mitaro imeziba na barabara zinazidi kuharibika, wananchi wanashindwa kufanya shughuli zao kwa uhuru kwa sababu ya ubovu wa miundombinu, tunaomba majibu ya uhakika ya kuwapa wananchi wetu" wamehoji Madiwani hao.
Awali akifungua baraza hilo Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha Maxmillian Iranqhe amedokeza akiwataka madiwani hao kutojadili suala la barabara kuwa, vifaa vimeagizwa vikifika wataambiwa.
"Vifaa vimeagizwa nje na vikiletwa tutaitana kuvipokea ili kazi ya matengenezo ya barabara na mitaro iendelee, bahati nzuri ukusanyaji wa mapato unaenda vizuri, hivyo ni imani yangu kwamba miradi yote itakamilika kwa wakati" ameeleza Iranqhe.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Arusha Felician Mtahengerwa akizungumza katika baraza hilo amewataka watendaji wote wanaohusika na miradi ya barabara wakiwemo TARURA na Watu wa manunuzi, kuikamilisha kwa wakati vinginevyo wataachia nafasi zao.
"Nawaambia madiwani muda wenu ni mchache, acheni kuwachekea hawa watawaangusha shimoni, muda ukifika mtaogopa kusimama majukwaani kunadi sera zenu kw sababu ya wazu wazembe wanaopokea fedha na kushindwa kuwajibika ipasavyo, maana wananchi wanawaangalia nyinyi, endeleeni kufumbia macho mambo haya mtaumia"ameongeza
" Kama hizo pesa zimeshatengwa ni miezi mitatu sasa kwa nini changamoto ziko palepale, sitamvumilia yeyote atakayetaka kurudisha nyuma jitihada za serikali" ameeleza Mtahengerwa.
Hata hivyo amewakumbusha madiwani kusimamia usafi wa mitaa, kuhamasisha ufungaji wa taa za barabarani, kupanda miti na kuibua wanaojihusisha na utengenezaji wa pombe haramu.
Post A Comment: