Na Mapuli Kitina Misalaba
Ligi ya Makamba Lameck maarufu kama Krismas Cup imeendelea kuchanja mbuga katika kata ya Salawe, ambapo leo Salawe FC wameibuka washindi wa mechi kali dhidi ya Solwa FC kwa ushindi wa goli moja.
Mfungaji wa goli pekee katika mechi hiyo ni Badala Masalu, aliyetikisa nyavu dakika ya 67, na kuteuliwa kuwa mchezaji bora wa mechi (Man of the Match).
Mgeni rasmi wa mechi ya leo Disemba 2, 2024 ni mdau wa michezo Paul Daudi (MC Niache Kona), amepongeza kiwango cha juu cha ligi hiyo huku akitoa shukrani za dhati kwa Makamba Lameck kwa kuandaa mashindano ambayo amesema ni chachu ya kuwasaidia vijana kupata fursa za ajira kupitia michezo.
Wadau wengine wa michezo pia wameeleza kuridhishwa na ubora wa ligi hiyo, huku baadhi ya wananchi wakishukuru kufurahia mechi hizo bila kutozwa kiingilio.
Kwa upande wake, msimamizi wa ligi hiyo, Mwalimu Emmanuel Enick Kijida, ametangaza ratiba ya mechi inayofuata, ambapo kesho Beya FC watavaana na Ngubalu FC katika mchezo mwingine wa kusisimua.
Kumbuka ligi hii, imeandaliwa na Makamba Mussa Lameck kupitia kampuni yake ya MCL inayojihusisha na biashara ya nafaka, ikiwa lengo ni kuibua vipaji vya michezo katika Mkoa wa Shinyanga na kuleta mshikamano wa kijamii.
Michezo hii, ambayo imeendelea kuwa kivutio kikubwa kwa wakazi wa Kata ya Salawe na maeneo ya jirani, si tu burudani bali pia ni jukwaa muhimu la kuwaunganisha vijana na kuwapa nafasi ya kuonesha uwezo wao wa kisoka.
Post A Comment: