Na WAF - Nkinga, Tabora
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amezindua rasmi mashine ya MRI inayotoa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya shinikizo la juu la damu, magonjwa ya moyo pamoja na majeraha makubwa ya mifupa na ubongo katika Hospitali ya Rufaa ya Nkinga, inayomilikiwa na kanisa la 'Free Pentecostal Church of Tanzania (FPCT).
Waziri Mhagama amezindua huduma hiyo leo Desemba 20, 2024 Mkoani Tabora, itakayowasaidia Watanzania wote hususani wanaoishi Kanda za Magharibi, Ziwa na Kati zinazojumuisha mikoa ya Tabora, Kigoma, Singida, Shinyanga na Simiyu.
"Tumezindua rasmi huduma za kipimo cha mashine ya MRI ambacho ni kipimo cha kibobezi kinachotoa huduma ya mionzi na sumaku kwa uchunguzi wa wagonjwa kwa wenye matatizo ya shinikizo la juu la damu, magonjwa ya moyo pamoja na waliopata majeraha makubwa ya mifupa na ubongo," amesema Waziri Mhagama.
Amesema, kipimo hicho kinawasadia madaktari kutoa matibabu sahihi na kwa wakati hivyo kuzuia madhara makubwa ambayo yangeweza kujitokeza ikiwemo kifo.
Aidha, Waziri Mhagama amesema Serikali ina wajibu wa kuhakikisha huduma hizi za kipimo cha MRI zinaingizwa katika utaratibu wa matibabu ya Bima ya Afya ya Taifa ili kuwawezesha wananchi wengi kupata huduma hizo kwa urahisi bila kikwazo cha fedha.
"Serikali kupitia Wizara imeanzisha utaratibu wa kuzipeleka huduma za kibingwa karibu zaidi na wananchi ambapo kambi za madaktari bingwa zijukanazo kama "Madaktari bigwa wa Dkt. Samia" ambao walitoa huduma katika halmashauri zote 184 kwa fani Sita (6) yakiwemo magonjwa ya ndani, magonjwa ya wanawake na uzazi, watoto, upasuaji, kinywa na meno na mifupa," amesema Waziri Mhagama.
Ameongeza kuwa katika ngazi ya hospitali za kanda na mikoa, fani zaidi ya 17 za mabingwa na wabobezi walishiriki kuwahudumia wananchi kupitia kambi mbalimbali na hivyo kambi hizi zitaendelea kufanyika ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kibingwa na kibobezi karibu na maeneo yao.
Pia, Waziri Mhagama ameahidi kutoa gari la dharura la kubebea wagonjwa (Ambulance) katika hospitali hiyo ikiwa ni hatua za kutatua changamoto inayoikumba hospitali hiyo ili kurahisisha huduma, hasa kwa akina mama wajawazito.
Waziri Mhagama ametoa wito kwa Watanzania wote kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo Kisukari, Magonjwa wa Moyo, Shinikizo la juu la damu kwa kufanya mazoezi na kuzingatia lishe bora na kuwahamasisha kufika kwenye vituo vya afya pindi wanaposikia mabadiliko yoyote ya kiafya ili kufanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu sahihi na kwa wakati.
Awali, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Nkinga Dkt. Titto Chaula amesema kuwa Hospitali hiyo ina madaktari bingwa 13 wakiwemo wabobezi wawili wa moyo pamoja na mifupa, lengo likiwa ni kusogeza huduma hizo karibu na wananchi ili wasipate tabu ya kufata huduma mbali na maeneo yao.
"Tunaishukuru sana Serikali inayoongonzwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuunga mkono, katika hospitali yetu kupitia Wizara ya Afya tumepokea vifaa mbalimbali ambavyo vinasaidia katika kuwahudumia wananchi wa wilaya ya Igunga na Nkinga katika mkoa wetu wa Tabora," amesema Dkt. Chaula. <This message was edited>
Post A Comment: