Na Okuly Julius _ Dodoma
Serikali imesema ili kuwahudumia wananchi kwa ufanisi ni vyema watumishi wa Umma kujifunza zaidi matumizi ya mifumo mipya ya TEHAMA kwa lengo la kuwafikia wananchi kwa ukaribu.
Kauli hiyo imetolewa leo Disemba 12,2024 jijini Dodoma na Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Xavier Daudi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea Kikao Kazi cha Mwaka cha Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Wizara, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Idara zinazojitegemea, Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali
"naomba kuwakumbusha kuwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (OR-MUUUB) ina majukumu mbalimbali kwa mujibu wa Hati ya Mgawanyo wa Majukumu kwa Mawaziri kama ilivyotangazwa katika Gazeti la Serikali Toleo Na. 619A & 619B la tarehe 30/8/2023. Moja ya majukumu hayo ni kusimamia Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma na Utawala wa Utumishi wa Umma, " ameeleza Bw. Daudi
Amesema katika kuhakikisha majukumu hayo yanatekelezwa kwa haraka na kwa ufanisi, Ofisi hiyo kila mwaka, hufanya Kikao Kazi cha Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Wizara, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Idara zinazojitegemea, Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali kwa lengo la:-
Moja : Kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu;
Mbili : Kukumbushana kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma mathalani; matumizi ya mifumo ya kidijitali ya e-Watumishi, e-Uhamisho, e-Utendaji, e-Mrejesho, HR Assessment.
Tatu : Kupeana maelekezo kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika utumishi umma kwa kuzingatia Shabaha na vipaumbele vya Taifa.
Pia Bw. Daudi amewataka Waajiri nchini kuwaruhusu Wakuu hao wa Idara kushiriki kikamilifu katika kikao kazi hicho ili kujifunza mbinu mbalimbali za kutoa huduma bora kwa wananchi na kupunguza malalamiko.
Amesema kutokana na umuhimu wa Kikao Kazi hicho, amewataka Wakuu wote wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu,
Kujisajili kwenye mfumo wa https://tsms.gov.go.tz na mwisho wa kujisajili ni tarehe 13 Desemba, 2024.
Pia amewataka Kufika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jiji la Dodoma uliopo katika Mji wa Serikali Mtumba tarehe 16 Disemba, 2024 kuanzia saa 10:00 Jioni ili kuchukua vitambulisho na makabrasha ya kikao
Naye Mkurugenzi wa Utawala wa Utumishi wa Umma Bi. Felister Shuli amesema Rasilimaliwatu ni nguzo ya Uendelezaji wa rasilimali zingine hivyo ni muhimu kujengewa uelewa.
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu SACP Ibrahim Mahumi amesema kuna baadhi ya changamoto ambazo zinaweza kujadiliwa katika kikao kazi hicho na kupatiwa ufumbuzi.
Kikao kazi hicho kinatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 17 hadi 19 Desemba, na kitaongozwa na Kaulimbiu isemayo "Kusimamia Sera na Sheria za Utumishi wa Umma kupitia Mifumo ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala ya Kidijitali iliyoboreshwa” na Mgeni Rasmi wakati wa Ufunguzi anatarajiwa kuwa Waziri wa Nchi - Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene.
Post A Comment: