๐Ashiriki Kongamano la Wafanyabiashara na Wawekezaji nchini humo
๐ Zaidi ya Wafanyabiasha na Wawekezaji 250 wakutana
๐ JNHPP yatajwa kuongeza uhakika wa uwepo wa umeme
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Kongamano la Wafanyabiashara na Wawekezaji nchini Saudi Arabia litaongeza uwekezaji kwenye Sekta ya Nishati kutokana na Tanzania kuzinadi fursa zilizopo kwenye maeneo mbalibali ikiwemo Gesi Asilia, Umeme na Nishati Safi ya Kupikia.
Mhe. Kapinga amesema hayo katika Kongamano la Wafanyabiashara na Wawekezaji zaidi ya 250 kutoka Tanzania na Saudi Arabia linalofanyika tarehe 18 na 19, Disemba, 2024 katika Mji wa Riyadh nchini Saudi Arabia.
Amesema kuwa, Kongamano hilo ni muhimu kwa upande wa Wizara ya Nishati na nchi kwa ujumla kwa kuwa linatangaza fursa zilizopo nchini katika uwekezaji kupitia Sekta ya Nishati ikizingatiwa kuwa kwa sasa Tanzania inavyanzo vingi vya kuzalisha umeme mwingi na wa uhakika likiwemo Bwawa la Julius Nyerere ambalo litazalisha jumla ya Megawati 2,115. M
" Kongamano hili litaendelea pia kujenga mahusiano mazuri kati ya Tanzania na Wadau kutoka Saudi Arabia katika Sekta ya Nishati." Amesema Kapinga
Akifungua Kongamano hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, aliwakaribisha wawekezaji kuwekeza nchini na kueleza kuwa Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji katika Sekta mbalimbali kupitia Sera nzuri, Misingi imara na Rafiki kwa wawekezaji iliyowekwa.
Aliwakaribisha wawekezaji hao kuwekeza katika nyanja mbalimbali ikiwemo Nishati, Madini, Viwanda, Biashara, Kilimo, Miundombinu pamoja na Uchumi wa Buluu.
Profesa Mkumbo alieleza kuwa Sekta ya Uwekezaji nchini kwa sasa inakua kwa kasi kubwa, ambayo imechagizwa na Sera nzuri zilizopo chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuhakikisha kuwa wawekezaji wengi wanakuja kuwekeza nchini ili kukuza uchumi na kuitangaza Tanzania kote ulimwenguni.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, Dkt. Mah’d Juma Abdalla amewaasa watanzania wanaoshiriki kongamano hilo kutumia vyema fursa hiyo kuitangaza vyema nchi yao na kutanua wigo wa biashara zao kwa kuwa nafasi hizo ni aghalabu kupatikana.
Amesema kila mshiriki ahakikishe anatimiza lengo lililompeleka katika nchi hiyo ili aweze kupata matokeo chanya katika sekta yake baada ya kongamano hilo kumalizika.
Mawaziri mbalimbali wanaohudhuria Kongamano hilo ni Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Jaffo, Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Madini, Antony Mavunde na Naibu Waziri wa nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Ajira na Uwekezaji Zanzibar, Sharif Ali Sharif.
Viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Taasisi zake wanaoshiriki Kongamano hilo ni Kamishna Msaidizi wa Petroli, Mhandisi Joyce Kisamo, Mkurugenzi Msaidizi wa Sera, Utafiti na Ubunifu, Oscar Kashaigiri na Meneja wa Biashara ya Mafuta wa kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Baraka Nyakutonya.
Post A Comment: