Na Mapuli Kitina Misalaba

Robo fainali ya kwanza ya Ligi ya Makamba Lameck (Krismas Cup) imefanyika leo Desemba 7, 2024 kwa ushindani mkali kati ya Sekondari Combine FC na Kano FC, ambapo Kano FC wameibuka washindi kwa bao 1-0 lililofungwa na Emmanuel Mchenya dakika ya 57.

Akizungumza kwa niaba ya msimamizi wa mashindano hayo, Placid Thomas amesema ligi hiyo itaendelea kesho kwa mchezo mwingine wa robo fainali kati ya Beya FC na Ikonongo FC (Mahakama).

Ametumia nafasi hiyo kuwahimiza wananchi na wapenzi wa michezo kujitokeza kwa wingi kushuhudia vipaji vya wachezaji wa Shinyanga.

Kocha wa Sekondari Combine FC amepongeza juhudi za vijana wake, akisema kuwa mashindano haya ni chachu ya kuwaandaa kwa mashindano mengine makubwa.

Pia, amemshukuru Makamba Lameck kwa kuwawezesha vijana kushiriki mashindano hayo na kumuomba aendelee kuandaa matukio kama haya katika siku zijazo.

Mashindano ya Krismas Cup, yanayodhaminiwa na Makamba Lameck kupitia kampuni yake ya MCL inayojihusisha na biashara ya nafaka, yanalenga kukuza vipaji vya michezo mkoani Shinyanga.

Fainali za mashindano hayo zinatarajiwa kufanyika tarehe 17 Desemba 2024, huku hamasa ikiendelea kuongezeka miongoni mwa timu shiriki na mashabiki wa michezo.



Share To:

Misalaba

Post A Comment: