Mkuu wa Kitivo cha Insia na Sayansi ya Jamii katika Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Dkt. Leticia Rwabishugi(katikati), amesema kuwa chuo hicho kimepanga kuanza kutoa masomo ya biashara na lugha ya kichina kwa ngazi ya Shahada na Shahada ya Uzamili, hatua  inayolenga kuzalisha wahitimu wenye ujuzi unaolingana na mahitaji ya soko la ajira, kutokana na fursa kubwa zinazopatikana katika masomo hayo.

Aidha, Dkt. Rwabishugi amebainisha kuwa Chuo kitaendelea kushirikiana na  Taasisi ya Confucius (Confucius Institute), kwa lengo la ktoa fursa kwa wanafunzi kupata ufadhili wa kwenda kusoma lugha ya kichina nchini China.

Dkt. Rwabishugi amesema hayo wakati wa hafla ya kusherehekea Sikukuu ya Majira ya Baridi ya kichina (Winter Chinese), iliyofanyika ndani ya Chuo cha Uhasibu Arusha na kuhudhuriwa na wadau wa lugha ya Kichina pamoja na wanafunzi wanaojifunza lugha hiyo.

Akizungumzia maendeleo ya masomo ya lugha ya kichina katika chuo hicho, amesema mwaka 2021 walianza kutoa masomo hayo kwa ngazi ya cheti wakiwa na wanafunzi wanne pekee, na  kufikia 2024 idadi  imeongezeka hadi wanafunzi 480 katika ngazi ya Cheti, Diploma ya Kwanza na ya Pili.

Amehitimisha kwa kuwashukuru wadau wanaosaidia kutoa mafunzo kwa vitendo, akisisitiza kuwa hatua hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kukuza ujuzi wa wanafunzi kuzungumza lugha ya Kichina kwa ufasaha, pamoja na kuwapa fursa za kuajiriwa na hata kujiajiri.

Baadhi ya wanafunzi wamesema  kujifunza lugha ya Kichina kumeongeza ujuzi wao wa mawasiliano na kuwapa matumaini ya kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi












Share To:

Post A Comment: