Na Benny Mwaipaja na Saidina Msangi, Saudi Arabia


DKT. NCHEMBA AKARIBISHA SAUDI ARABIA KUWEKEZA TANZANIA

Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameikaribisha Saudi Arabia kuwekeza Tanzania katika fursa mbalimbali zikiwemo utalii, kilimo, madini, uendelezaji wa miundombinu pamoja na uchumi wa buluu.

Dkt. Nchemba alitoa mwaliko huo alipokutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Wizara ya Uchumi na Mipango wa Saudi Arabia, Eng. Ammar Naqadi, Kando ya Mkutano wa Jukwaa la Biashara na Uwekezaji, lililoandaliwa na Ubalozi wa Tanzania, kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Shirika la Kuendeleza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), lililofanyika hivi karibuni Mjini Riyadh nchini Saudi Arabia.

Alibainisha kuwa Tanzania inaendelea na mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ambapo imeshakamilika kipande kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma na ujenzi unaendelea kwa vipande vinavyoelekea Mwanza na DRC kupitia Burundi hivyo ni fursa kwa Saudi Arabia kuwekeza katika miundombinu hiyo ambayo itachochea ukuaji wa bishara kati ya Saudi Arabia, Tanzania na nchi za Afrika Mashariki.

‘‘Bado tunakusanya rasilimali tunatamani wewe na taasisi yako kuona namna ambavyo tunaweza kushirikiana katika ujenzi na uendeshaji wa mradi huu wa reli ya kisasa ambao utahusisha na sekta binafsi ikiwemo katika usafirishaji wa mizigo na safari za kila siku’’, alieleza Dkt. Nchemba.

Aidha, Dkt. Nchemba alieleza kuwa Tanzania ina fursa katika sekta ya kilimo ambapo ina ardhi ya kutosha na yenye rutuba kuweza kuzalisha mazao ya aina mbalimbali kwa wingi hivyo ni vema Saudi Arabia ikatazama fursa katika sekta hiyo muhimu.

‘’Tunaweza kushirikiana katika kilimo ikiwemo usalishaji wa ngano, mafuta ya kupikia pia tuna ranchi ambazo zinaweza kutumika kuzalisha nyama za kutosha na hivyo kupata mazao na bidhaa za kusafirisha nje ya nchi jambo litakalotunafaisha sisi pamoja na ninyi pia’’, alifafanua Dkt. Nchemba.

Aliongeza kuwa Tanzania pia ina aina ya madini ambayo yanapatikana Tanzania tu hivyo hiyo ni fursa muhimu kwa Saudi Arabia kuweza kushirikiana na Tanzania kuwekeza katika sekta hiyo kwa kujenga viwanda vya kuchakata madini ili kuyaongezea  thamani.

Uwekezaji huo utawezesha kubadilishana uzoefu na Saudi Arabia wa rasilimali watu pamoja na teknolojia itakayoisaidia Tanzania katika kupiga hatua ya maendeleo ya kiuchumi haraka zaidi.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, alisema kuwa Zanzibar ina fursa zinazoweza kutumiwa na Saudi Arabia ikiwemo sekta ya utalii wa fukwe za asili zilizopo Zanzibar, fursa ya uvuvi wa kina kirefu  na uchakataji wa mazao ya uvuvi pamoja na  uwepo wa vyanzo vya gesi   na mafuta vilivyogunduliwa ni fursa muhimu kwa Saudi Arabia kutokana na uzoefu wake katika sekta hiyo.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Uchumi na Mipango wa Saudi Arabia, Eng. Ammar Naqadi, alisema kuwa Saudi Arabia iko tayari kushirikiana na Tanzania katika uendelezaji wa miundombinu ya reli ili kurahisha usafirishaji wa watu, mazao na mizigo ili kuchochochea ukuaji wa biashara ambapo ushiriki wa sekta binafsi ni muhimu katika kufanikisha biashara kati ya nchi hizo mbili.

Alisema nchi hiyo iko tayari kushirikiano na Tanzania katika fursa za kuendeleza sekta ya madini, kilimo, mafuta na gesi, utalii, uchakataji wa mazo ya bahari miundombinu pamoja na utalii ambapo wataandaa timu ya wataalamu kwa kushirikiana na Sekta binafsi kutembelea Tanzania kujionea fursa za uwekezaji katika sekta hizo ili kujiridhisha na mazingira ya fursa za Tanzania ili kuweza kuwekeza.

Alisisitiza kuwa katika kufanikisha ukuaji wa biashara baina ya Tanzania na Saudi Arabia suala la utozaji kodi mara mbili ni muhimu kufanyiwa kazi ili kuwawezesha wafanyabiashara kutopata changamoto wafanyapo biashara kati ya pande hizo.

Katika kikao hicho Dkt. Nchemba aliambatana na Mawaziri wenzake wawili, akiwemo Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, Mhe. Dkt. Moh’d Juma Abdalla.





Share To:

Post A Comment: