Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amekabidhi vitendea kazi kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii vyenye thamani ya Shilingi Milioni 674.3 kwa mikoa Saba ambayo ni Njombe, Pwani, Kigoma, Ruvuma, Songwe, Lindi pamoja na Kagera.
Waziri Mhagama amekabidhi vitendea kazi hivyo leo Januari 3, 2025 akiwa mkoani Kagera, mkoa ambao umewakilisha mikoa mengine Sita itakayotoa huduma za afya kwa wananchi ikiwemo elimu juu ya magonjwa yasiyoambukiza na magonjwa ya milipuko.
"Vitendea kazi vilivyokabidhiwa ni pamoja na viatu maalum vya kazi, miamvuli, mabegi pamoja na sare maalum zitakazowatambulisha kuwa wao ni wahudumu wa afya ngazi ya jamii watakaokuwa wawili katika kila kitongoji (mwanamke na mwanaume)," amesema Waziri Mhagama.
Waziri Mhagama amesema, mpango huo wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii ni mpango wa Taifa unaoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, lengo likiwa ni kuhakikisha hadi ifikapo mwaka 2028 Tanzania inakuwa na wahudumu hao wapatao 137,294 nchi nzima ili kupunguza magonjwa.
Aidha, Waziri Mhagama amesema katika kipindi kifupi cha uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassa, Serikali imewezesha uwepo wa dawa pamoja na vifaa tiba ikiwemo vifaa vya uchunguzi ambavyo vinatumia tekinolojia ya hali ya juu.
"Sasa hivi kuna ongezeko la mashine ya uchunguzi wa magonjwa MRI 14, CT-Scan 45, Digital X- Ray 439, Ultrasound zaidi ya 600 pamoja na Pet-Sacan 1 mpya yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 18 ambayo tumeifunga pale kwenye Taasisi ya Saratani Ocean Road kwa ajili ya wagonjwa wa kansa," amesema Waziri Mhagama.
Waziri Mhagama amesema vifaa hivyo vinahitaji wataalam wabobezi, hivyo Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa Shilingi Bilioni 30 ili kusomesha wataalam bingwa na wabobezi katika masuala ya afya ikiwemo madaktari bingwa wa mionzi na usingizi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Hajat Fatma Mwasa ameishukuru Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Sekta ya Afya kwa uendelea kuboresha miundombinu pamoja na upatikanaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba ambavyo vimeweza kuwahudumia wananchi wa mkoa huo katika masuala ya afya.
"Hospitali yetu ya Rufaa ya Bukoba inapokea wagonjwa zaidi ya 300 kwa siku kwakuwa tunao madaktari bigwa 12 wanaokidhi katika fani mbalimbali, tunatoa shukurani za dhati kwa Mhe. Rais Dkt. Samia kwa kuimarisha huduma za afya kwa wagonjwa ikiwemo wagonjwa mahututi, na kwa sasa hospitali yetu inatoa huduma kama zinazotolewa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili," amesema Mhe. Mwasa.
Post A Comment: